WAKAZI wa Jiji la Dodoma wametakiwa kuwa na nyaraka za ujenzi hususan ramani na kibali cha ujenzi katika eneo la kazi (site) ili kuepusha usumbufu wakati wa zoezi la ukaguzi wa majengo mbalimbali ikiwemo ya makazi unaofanywa na wataalamu wa Mipango Miji wa Halmashauri ya Jiji hilo.
Rai hiyo imetolewa na Afisa Mipango Miji wa Jiji la Dodoma, Aisha Masanja wakati wa zoezi la ukaguzi wa majengo katika Kata ya Iyumbu Jumatatu hii Julai 27, 2020.
Ukaguzi huo uliofanywa na Wakuu wa Idara wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika Kata mbalimbali ulibaini kasoro kadhaa ikiweno ujenzi holela na kutokuwepo kwa nyaraka za msingi katika eneo la ujenzi kama ramani na vibali.
Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, Masanja alitoa rai kwa wananchi wanaofanya ujenzi kuhakikisha wanakuwa na vibali vya ujenzi na siyo kujenga holela na kuharibu taswira ya Jiji la Dodoma.
“Nakala ya ramani ya jengo lako pamoja na kibali lazima viwepo katika eneo la kazi ili Halmashauri inapofanya ukaguzi ijiridhishe na kazi ya ujenzi iendelee bila usumbufu, vinginevyo ujenzi utasimamishwa mpaka muhusika atakapo wasilisha nyaraka hizo katika Ofisi za Halmshauri ya Jiji kwa uhakiki” alisema Masanja.
Baadhi ya wakazi wanaoendelea na ujenzi na kukaguliwa wakati wa zoezi walikiri kupata elimu hiyo ya kuwa na nakala za nyaraka hizo katika eneo la ujenzi ili kuepuka usumbufu wakati wa ukaguzi wa majengo yao.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.