Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Magufuli leo tarehe 13 Oktoba, 2020 ameshuhudia kampuni ya Twiga Minerals na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) likitoa gawio kwa Serikali kutokana na faida katika biashara ya madini.
Halfa ya utoaji wa gawio hili imefanyika katika ukumbi wa kituo cha kimataifa cha mikutano cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam ambapo kampuni ya Twiga Minerals imekabidhi Dola za Marekani Milioni 40 (sawa na takribani shilingi Bilioni 100 za kitanzania) na STAMICO imekabidhi shilingi Bilini 1.1 kwa Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango.
Aidha, katika hafla hiyo wachimbaji wadogo wa madini kupitia chama chao (FEMATA) wametoa tuzo kwa Mhe. Rais Magufuli kwa kutambua mchango wake mkubwa wa kulinda maslahi ya wachimbaji wadogo na maslahi ya Watanzania katika rasilimali yao ya madini.
Waziri wa Madini, Mhe. Dotto Biteko amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa dhamira yake ya dhati na mwongozo wake katika usimamizi wa madini ambao umesaidia kubadili sekta ya madini kutoka sekta iliyofichwa na isiyo na maslahi kwa Watanzania na kutwa sekta inayofanyika kwa uwazi na inayowanufaisha Watanzania kwa kuchangia fedha nyingi katika pato la Taifa, kutoa ajira na kustawisha jamii.
Mhe. Waziri Biteko ametoa mfano kuwa kati ya mwaka 2015/16 na mwaka 2019/20 mapato ya madini yameongozeka kutoka shilingi Bilioni 168 hadi shilingi Bilioni 528 na kwa sehemu kubwa shughuli za madini zinafanywa na Watanzania wanyewe badala ya kufanywa na wageni kama ilivyokuwa zamani.
Katika hotuba yake, Mhe. Rais Magufuli ameelezea kufurahishwa kwake na mafanikio makubwa ambayo Tanzania imeyapata baada ya kuchukua hatua za kutunga sheria mpya ya madini kudhibiti wizi na utoroshaji wa madini na kunzisha masoko ya madini na ameewakata Watanzania wote kutembea kifua mbele kwa kuwa sasa madini yao yameanza kuwanufaisha.
Mhe. Rais Magufuli amesema Tanzania imejaliwa kuwa na utajifiri wa aina mbalimbali za madini kama gesi na mafuta hivyo ni wakati wa Watanzania kuamka na kuchamgamkia fursa za uchimbaji na uwekezaji katika rasilimali hizo bila kujali hadhi ya mtu, kampuni ama taasisi, ilimradi hawavunji sheria na wanalinda maslahi ya Taifa kwa kulipa kodi na tozo mbali mbali za kisheria.
Amewashangaa Watanzania ambao walikuwa wakipinga hatua zilizochukuliwa na Serikali kurekebisha dosari zote zilizosababisha Watanzania kutonufaika na madini yao ikiwemo kukamata makinikia ya dhahavu, kudhibiti wizi na utoroshaji, kupitia upya mikataba ya madini, kudai fidia na kutunga sheria zilizoiwezesha nchi kuwa na umiliki wa asilimia 16 katika migodi ya madini na kupata mgao wa 50/50 katika faida ya biashara ya madini.
Mhe. Rais Magufuli ameipongeza kampuni ya Barrick Gold ambayo ilikubali kuingia katika majadiliano na Serikali na matokeo yake kuundwa kwa kampuni ya Twiga Minerals ambayo leo imekabidhi gawio la shilingi Bilioni 100, na pia ameipongeza kamati iliyoongozwa na Prof. Palamagamba Kabudi ambayo iliiwakilisha Serikali katika majadiliano hayo, kwa kutekeleza jukumu hilo kwa uzalendo mkubwa licha ya kuzingirwa na vishawishi vya rushwa na hatari za kiusalama.
Aidha, Mhe. Rais Mafgufuli amesisitiza kuwa Tanzania ni mahali salama pa uwekezaji na ametoa wito kwa wafanyabiashara na wawekezaji mbalimbali wa ndani na nje ya nchi kuja kuwekeza hapa nchini katika sekta mbalimbal ikiwemo madini, na kwamba Serikali itakuwa tayari wakati wote kutoa ushirikiano utakaofanikisha uwekezaji huo ilimradi kuwepo mazingira ya mwekezaji kupata na Serikali kupata (win-win).
Mhe. Rais Magufuli amewashukuru viongozi wa Dini na Watanzania wote kwa maombi na dua kwa Taifa na amewataka kuendelea kufanya hivyo kwa kuwa Taifa linalosimama na Mungu hufanikiwa, kama ambavyo Tanzania imefanikiwa katika maeneo mengi ikiwemo kuepusha ugonjwa wa Corona (Covid-19) na kusimama kidete kutetea maslahi ya Watanzania.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.