Waziri Dkt. Ndumbaro awaasa wananchi wafanye matumizi endelevu ya misitu badala ya kukata miti ovyo hali inayoweza kusababisha mabadiliko ya tabianchi.
Dkt. Ndumbaro ametoa rai hiyo jana wakati akizungumza na wadau mbalimbali mara baada ya kushiriki zoezi la upandaji miti katika eneo la Iyumbu jijini Dodoma.
Alibainishata kuwa asilimia 54 ya eneo la nchi yetu ambayo ni sawa na hekta 400 ni misitu, hivyo kila mwananchi analo jukumu la kuitunza na kuendelea kupanda miti mingine ili Tanzania iendelee kuwa ya kijani na kuleta faida.
“Ndugu zangu faida za misitu tunazijua, misitu ni mali kwa sababu watu wanaoishi Mafinga mkoani Iringa na maeneo mengine misitu ndio biashara yao na hata kule nchini Norway misitu inachangia sana kwenye GDP (pato la taifa),” alisema.
Aidha, Waziri Dkt. Ndumbaro aliongeza kuwa kutokana na umuhimu wa misitu hiyo asilimia 3.5 ya Pato la Taifa inachangiwa na sekta hiyo hapa nchini hivyo alisisitiza umuhimu wa kuilinda.
Hivyo, aliipongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuratibu Wiki ya Mazingira kuelekea kilele cha uzinduzi wa Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021 na kushiriki zoezi la upandaji miti kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), katika msimu huu wa mvua waliotoa miche ya miti mbalimbali ambayo imepandwa leo katika eneo la Greenpark, Iyumbu jijini Dodoma.
Alisema miti hiyo itasaidia kukabiliana na madhara yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi ambayo yameendelea kushuhudiwa kutokana na mabadiliko yake kuja na athari hasi nyingi zikiwemo kuongezeka kwa joto duniani, kuongezeka kwa baridi, pamoja na kubadilika kwa misimu ya hali ya hewa.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Mary Maganga alitoa wito kwa wananchi kupanda miti katika maeneo yao ili kuendelea kuifanya nchi kuwa ya kijani na mfano wa kuigwa.
Bi. Maganga alisema zoezi la upandaji ni kielelezo cha kutoa hamasa na kuhamasisha maeneo mengine nchi nzima kupata uelewa kuhusu dhana nzima ya kuifanya nchi nzima kuwa ya kijani na ya mfano kupitia kampeni ya Kijanisha Dodoma.
Pia aliwashukuru wadau mbalimbali wa mazingira waliojitokeza katika zoezi hilo, hatua itakayoleta hamasa kwa wananchi ili waweze kufanya shughuli za upandaji miti na kuhifadhi mazingira kuwa sehemu ya maisha yao.
Nae Kamishna wa Uhifadhi kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Prof. Dos. Santos Silayo alisema nchi yetu imejaliwa kuwa na misitu ya aina mbalimbali ikiwemo ya kupanda na kuota kwa asili.
Prof. Silayo aliwataka wananchi kuwa na utamaduni wa kuitunza misitu iliyopo kwani ina mchango mkubwa katika sekta ya viwanda ambayo imekuwa kwa kasi kubwa hapa nchini.
Aliongeza kusema kuwa katika miaka mitatu iliyopita tulishuhudia viwanda takriban 800 vikiwemo vya kati na vikubwa vikianzishwa sambamba na ukuaji wa teknolojia huku akitolea mfano wa nguzo za umeme zinazozalishwa hapa nchini kutokana na misitu.
Kamishna huyo alisema Ukuaji wa viwanda umekwenda kwa kasi kubwa na hata tunashuhudia viwanda vya mkaa mbadala ambavyo vyote vinaleta mchango mkubwa katika kuhifadhi mazingira.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.