MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amefungua mkutano mkuu wa nne wa Mtandao wa Sala na Maombi ya Kitaifa na Kimataifa katika Ukumbi wa Morena Jijini Dodoma huku akiwataka watanzania kuendelea kuwa wamoja kwa kuzingatia maadili,uadilifu na misingi ya utawala bora.
Dkt. Mpango ameyasema hayo jana Jijini hapa wakati wa mkutano huo ulioandaliwa na Taasisi ya Kingdom Leadership Network Tanzania,uliotanguliwa na maombi ya kuliombea Taifa na Viongozi kwa ujumla kwa lengo la kuiongoza nchi kwa misingi ya kufuata utawala bora na uadilifu .
Mkutano huo wa kitaifa umeshirikisha viongozi mbalimbali wa kiserikali ndani na nje ya nchi pamoja na Viongozi wa Dini.
Akiongea katika Mkutano huo alisema Serikali ya awamu ya sita ya Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kufuata misingi ya utawala bora na utawala wa Sheria.
Alisema kuwa wao kama Serikali watahakikisha wanafuata misingi ya utawala bora kwa kuzingatia uwajibikaji,uwazi na uadilifu kwa lengo la kuleta haki kwa watu wanaowaongoza.
Katika hatua nyingine amesema kuwa katika kuelekea uchumi wa viwanda, Serikali itajikita katika ushindani wa kibiashara pamoja na kuondoa vikwazo kwa wawekezaji huku akitumia fursa hiyo kuwa wakaribisha wawekezaji wa nje ya nchi kuja kuwekeza nchini.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Taasisi ya Kingdom Leadership Network Tanzania, (KLNT)ambao ndiyo waandaji wa Mkutano huo Fredrick Ringo alisema dhumuni la mkutano ni kuombea nchi kila mwaka kwa kushirikisha viongozi mbalimbali wa serikali, wabunge na Wafanyabiashara.
Alisema, kwa kuliombea Taifa, Mwenyezi Mungu huepusha dhoruba na kuifanya nchi kuendelea kuwa na utulivu hali itakayowezesha wananchi wake kuwa huru katika kujijenga kiuchumi.
"Kupitia Mkutano huu,tunamwomba Muumba wetu aisaidie Tanzania hasa viongozi waliopo madarakani waweze kutenda haki kwa kufuata misingi ya utawala bora katika kuongoza wananchi,"alisema.
Naye Dkt. Charles Sokile ambaye ni Mkuu wa Chuo cha Biashara cha Joseph na ni Mkurugenzi wa mahusiano ya kimataifa wa Taasisi hiyo alisema kupitia mkutano huo wamepata fursa ya kutangaza rasmi uhusianao wa kibiashara na marekani.
Alisema hali hiyo itasaidia kuunganisha biashara za Tanzania na marekani katika maeneo makubwa sita ikiwemo utalii pamoja na kutangaza mpango rasmi wakuanzisha kituo kidogo cha biashara.
"Hii itasaidia biashara zisizo rasmi ziwe rasmi kwa maendeleo ya uchumi wa Taifa," alisisitiza.
Kutokana na hayo naye Sophia Mwakagenda Mbunge wa Viti maalum,alieleza umuhimu wa kuwa na uwazi na uwajibikaji kwa viongozi hasa katika kumtanguliza mungu kwa maombi.
Alisema, pamoja na changamoto Dunia inazozipitia lazima watu wasimame pamoja kwa kipindi chote bila kujali itikadi za kidini au siasa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.