RAI imetolewa kwa wananchi wote wa Mkoa wa Dodoma na nje ya Mkoa huo kufuga nyuki kwa kutumia mbinu rafiki kwa mazingira ili kuimarisha afya na kujiongezea kipato.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya kitaifa kuelekea kilele cha siku ya Nyuki duniani 2024 katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma.
Lengo kuu la kuanzishwa kwa madhimisho hayo ni kutambua mchango wa Sekta ya Nyuki katika maisha ya mwananchi mmoja mmoja, Taifa na Dunia kwa ujumla.
"Siku hii ni sehemu ya kuenzi jitihada za mwanzilishi wa ufugaji Nyuki Bwana Anton Jana, raia wa nchi ya Slovenia ambapo nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa ziliidhinisha na kutangaza rasmi tarehe 20 Mei ya kila mwaka kuwa siku ya Nyuki Duniani itakayoadhimishwa na kila nchi mwanachama wa Umoja huo kulingana na mazingira ya nchi husika" Ameeleza Mhe.Senyamule
Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa amesema maadhimisho hayo yanatoa fursa kwa wafugaji nyuki, wajasiriamali na wafanyabiashara wa mazao ya nyuki na wadau wengine wa sekta hiyo kukutana kwa lengo la kujengeana uwezo wa namna bora ya kuendeleza Sekta hiyo katika Mkoa wa Dodoma na Taifa kwa ujumla.
Kwa Upande Wake, Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki, Wizara ya Maliasili na Utalii Bw. Deusdedit Bwoyo amesema Mkoa wa Dodoma una zaidi ya mizinga 18,000 ya nyuki yenye uwezo wa kuzalisha zaidi ya kilo 135,000 za asali, kiwango hicho bado ni kidogo licha ya uwepo wa eneo la ukubwa wa zaidi ya hekta Milioni 1 linalofaa kwa ufugaji Nyuki.
Maadhimisho hayo yanachagizwa na kauli mbiu "Nyuki kwa Afya na maendeleo, tuwatunze". Kauli mbiu hii inatukumbusha mchango wa mdudu Nyuki katika afya zetu kutokana na matumizi ya mazao mengi anayozalisha pamoja na kujipatia kipato kupitia mazao hayo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.