WATANZANIA wametakiwa kulipa Kodi ikiwa ni takwa la kisheria katika nchi yeyote yenye maendeleo. Hayo yamebainishwa leo Mei 30, 2024 na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule kwenye kikao cha uzinduzi wa kampeni ya utoaji Elimu kwa umma na kuitambulisha ofisi ya usuluhishi wa Malalamiko na taarifa za Kodi.
Kikao hicho kilichofanyika kwenye ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma jengo la Mkapa Jijini Dodoma, kimelenga kuitambulisha Taasisi hiyo kwa umma na kutambulisha majukumu yake kwani inafanya kazi na jamii kwa ujumla.
“Uwepo wa ofisi hii unatoa fursa ya usimamizi wa Kodi. Wananchi, tumieni fursa hii kutatua changamoto zenu za Kodi. Hakikisheni munamlipa Kodi na kupata huduma kwani ni wajibu. Kulipa Kodi ni jambo la kihistoria na Kiimani pia kwani hakuna nchi inaweza kuendelea bila Kodi” Mhe. Senyamule.
Alizungumza wakati wa kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini Mhe. Jabir Shekimweri, amemshukuru Rais kwa kusukumwa na kushawishika kuanzisha jambo hili kwani ni utashi wa hali ya juu. Amesema kuwa, Taasisi hii itasaidia ukusanyaji Kodi wa halali na wenye kufuata utaratibu kwani makadirio mengi ya Kodi huzalisha migogoro.
Hata hivyo, Kaimu msuluhishi wa mabadiliko ya Kodi Bw. Godwin Barongo, ameelezea dhumuni la kuanzishwa kwa Ofisi ya Msuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi kuwa ni kushughulikia Malalamiko na Taarifa za Kodi yanayotokana na usimamizi wa Sheria na taratibu za Kodi unaofanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania, Kamishna Mkuu na Watumishi.
Aidha, uanzishwaji wa ofisi hiyo, unategemewa kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za ukusanyaji wa Mapato ikiwa ni pamoja na kuhusika kwenye kupokea, kuhakiki, kusajili na kutatua Malalamiko na taarifa za Kodi.
Kampeni ya utoaji Elimu kwa umma na kuitambulisha ofisi ya Msuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi Tanzania (Tax Ombudsman Service Tanzania - TOST) inatarajiwa kufanyika Tarehe 6 June, 2024 kwenye viwanja vya Nyerere Square Jijini Dodoma na itaongozwa na kauli mbiu, “Kataa ukwepaji Kodi, Kataa Kodi za dhulma”.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.