MKURUGENZI wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru (wa kwanza kushoto pichani juu) amewataka Maafisa Watendaji wa Kata na Mitaa kusajili malalamiko ya wananchi katika rejista ya malalamiko, wakielezea jinsi walivyoyatatua na kuwasilisha ofisini kwake yale ambayo yanahitaji utatuzi kwa ngazi ya Halmashauri.
Mafuru alitoa agizo hilo alipokuwa akiongea na wananchi wa Kata ya Nala katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma hivi karibuni.
Mafuru alisema kuwa agizo hilo ni kwa watendaji wote wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, “Changamoto nyingine zinasababishwa na watendaji wa Kata. Mtendaji anatakiwa kuangalia kwenye rejista yake kuna malalamiko mangapi, yaliyotatuliwa, mangapi yanayoendelea kufanyiwa kazi na yale yanayohitaji utatuzi wa ngazi ya Halmashauri anamuandikia Mkurugenzi kuomba wataalam kuja kutatua malalamiko hayo huku huku. Haipendezi wananchi kufunga safari kwenda makao makuu ya Halmashauri kutafuta utumbuzi wa matatizo ambayo yanaweza kutatuliwa katika maeneo yao” alisema Mafuru kwa msisitizo.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma alifanya ziara ya kikazi katika Kata ya Nala juzi tarehe 12 Septemba, 2020 ili kusikiliza na kutatua kero za wananchi katika utaratibu aliojipangia wa kutembelea Kata na Mitaa kusikiliza na kutatua kero za wananchi.
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Joseph Mafuru (wa pili kushoto waliokaa mbele), Mtendaji wa Kata ya Nala Mkumi Bhujabi Matage (kushoto kwa mkurugenzi), Mwenyekiti wa Mtaa wa Nala Herman Yohana Masila (wa kwanza kushoto waliokaa mbele), maafisa wa Jiji (waliokaa nyuma ya meza kuu) na wananchi wa Nala (hawapo pichani) wakimsikiliza Kaimu Mkuu wa Idara ya Ardhi, Mipango Miji na Maliasili Emelya Chaula (kulia) akitoa ufafanuzi juu ya hoja zilizohusu ardhi.
Wananchi wa Nala wakimsikiliza Mkurugenzi wa Jiji Joseph Mafuru (hayupo pichani) na kisha wakapata nafasi ya kutoa kero zao kwa ajili ya utatuzi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.