KAIMU Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Balthazar Ngowi amewataka watendaji wa Kata kuwa mfano kwa kuwahi kazini na kupinga vitendo vya rushwa katika maeneo yao ya kazi ili kuwezesha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Kauli hiyo aliitoa hivi karibuni alipokuwa akifungua mafunzo maalum ya kuwajengea uwezo maafisa watendaji wa Kata ili waweze kusimamia afua za Lishe katika Kata zao tukio lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Ngowi alisema kuwa watendaji wa Kata wanatakiwa kuwahi kazini na kutoa huduma bora kwa wananchi. “Nasema hili, siyo kwamba watendaji wote mnachelewa, hapana. Lakini nalisisitiza kwa sababu wapo watendaji wachache wanaochelewa na kuchelewa kwao kunasababisha ucheleweshaji wa kutoa huduma” alisema Ngowi. Aidha, aliwataka watendaji hao kusimamia na kuhamasisha ulipaji kodi ya serikali katika Kata. Serikali inaendeshwa kutokana na kodi, ambayo inapokusanywa vizuri inapelekwa katika kuboresha utoaji wa huduma za jamii, aliongeza.
Ngowi, ambaye pia ni mkuu wa idara ya Utumishi na Utawala katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma aliwataka watendaji hao kujiepusha na vitendo vya rushwa. “Mnajua nyie maafisa watendaji ni watawala katika maeneo yenu. Na sifa ya mtawala ni kutokuwa na viashiria vya rushwa. Mnatakiwa kusimamia haki katika utendaji wenu wa kazi ili wananchi wapate huduma bora” alisisitiza Ngowi.
Akiongelea tatizo la lishe kwa watoto katika Kata, alisema kuwa watendaji ni sehemu ya kuchochea tatizo hilo. Aidha, aliwataka kuhamasisha na kusimamia masuala ya lishe vizuri katika Kata zao.
Kwa upande wake Afisa Lishe wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Semeni Eva Juma alisema kuwa hali mbaya ya utapiamlo inasababishwa na ulishaji duni, maradhi ya mara kwa mara na huduma hafifu za malezi na makuzi ya awali ya watoto wadogo. “Utapiamlo unachangia maradhi, vifo na uchelewaji wa ukuaji wa mwili na maendeleo ya akili kwa watoto” alisema Juma.
Akiongelea malengo ya mkataba baina ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji na watendaji wa Kata, alisema kuwa lengo kubwa ni kufanikisha suala la kuboresha hali ya lishe na kupunguza athari za utapiamlo katika jamii. Malengo mengine aliyataja kuwa ni kuhakikisha jamii kupitia uongozi wa Kata inashiriki ipasavyo katika kupanga, kutekeleza na kufuatilia maendeleo ya utekelezaji wa mpango wa Halmashauri na afua za lishe.
Akiongelea mafunzo hayo, afisa mtendaji Kata ya Hombolo Makulu, Aletas Bakindikile alisema kuwa uelimishaji ulikuwa mzuri. “Kwa upande wangu ni mambo yanayoelezeka kila siku katika jamii, hivyo sijaona jambo geni bali kutukumbushia tuendelee kutoa elimu ya lishe ili jamii nzima na vizazi vyetu viendelee kunufaika kupitia elimu ya lishe” alisema Bakindikile.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.