MAAFISA watendaji wa kata katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma wametakiwa kuibeba agenda ya Lishe kwa uzito unaostaili ili kufikia malengo ya Serikali ya kulifanya tatizo la Lishe kuwa historia nchini.
Kauli hiyo ilitolewa na mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Lucas Mbise (pichani juu aliyesimama) alipokuwa akifungua kikao kazi cha tathmini ya Mkataba wa Lishe kwa Maafisa watendaji wa Kata kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Idara ya Afya Jiji la Dodoma.
Mbise alisema kuwa anawapongeza maafisa hao kwa utekelezaji wa Mkataba wa Lishe katika Wilaya ya Dodoma. “Nina taarifa kuwa mmekuwa mkifanya mafunzo na vikao mbalimbali vya elimu ya Lishe. Pamoja na kufanya vizuri katika utekelezaji wa Mkataba wa Lishe kwenye kata zenu, mkaongeze bidii. Yale tunayojifunza tuyafanyie kazi kadri inavyotakiwa ili kutoa matokeo chanya. Tuichukulie ajenda ya lishe kwa uzito unaostahili” alisema Mbise.
Mbise ambae pia ni Afisa Tarafa wa Tarafa ya Zuzu katika Wilaya ya Dodoma, aliwataka maafisa watendaji wa kata kutoa elimu ya umuhimu wa siku 1,000 kwa mtoto. “Nichukue nafasi hii kutoa rai kwenu, nendeni mkatoe elimu ya umuhimu wa siku 1,000 kwa mtoto vizuri katika muktadha wa lishe. Elimu ifike kwa wananchi, kila mkutano uwe na agenda ya lishe” alisema Mbise.
Mwakilishi huyo wa Mkuu wa Wilaya aliwataka maafisa watendaji hao kusimamia suala ya lishe ya watoto katika kata zao. “Kila mtu anahitaji kuwa na watoto wenye akili na ufahamu mzuri, licha ya changamoto za kiuchumi. Jinsi ambavyo ungependa watoto wako wawe, tamani hivyo hivyo, kuona watoto kwenye jamii unayoiongoza wakiwa na ufahamu mzuri” alisema Mbise.
Kwa upande wake mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Gerald Ruzika alisema kuwa lishe ina mchango mkubwa katika mustakabali wa mwanadamu. “Sisi Maafisa Watendaji wa Kata tunasimamia maelekezo ya Serikali huko katika kata na mitaa. Hivyo, twende tukayatekeleze kwa ufanisi mkubwa” alisema Ruzika.
Naye, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Andrew Method alisema kuwa Maafisa Watendaji wa Kata ni watu muhimu sana katika maendeleo ya halmashauri na wananchi wake. “Mikataba hii imesainiwa leo sasa nendeni kuitekeleza” alisema Dkt. Method.
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Gerald Ruzika (aliyesimama) alipokuwa akizungumza wakati wa kikao cha tathmini ya Mkataba wa Lishe kwa Maafisa watendaji wa Kata za Jiji la Dodoma.
Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Lucas Mbise (kulia) na mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Gerald Ruzika (kushoto) wakimuangalia Afisa Mtendaji wa Kata ya Mpunguzi alipokuwa akisaini Mkataba wa Lishe.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.