MAAFISA Watendaji wa Kata katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma wametakiwa kusimamia utekelezaji wa afua za lishe katika Kata zao ili kukabiliana na hali duni ya lishe.
Kauli hiyo ilitolewa na kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Balthazar Ngowi alipokuwa akifungua mafunzo maalum ya kuwajengea uwezo maafisa watendaji wa Kata ili waweze kusimamia afua za lishe katika Kata zao leo katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri.
Ngowi alisema kuwa suala la lishe ni agenda ya kitaifa. Halmashauri ya Jiji inalipa suala ya lishe umuhimu mkubwa ili kuondokana na tatizo la udumavu, aliongeza. Alisema kuwa muelekeo wa Taifa ni uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2025. Taifa haliwezi kuendelea iwapo watu wake wanakabiliwa na tatizo la udumavu. “Maafisa watendaji wa Kata mnawajibu wa kuhakikisha tatizo la lishe vinapatiwa ufumbuzi katika Kata zenu kwa kushirikiana na maafisa watendaji wa mitaa na vijiji” alisema Ngowi.
Akiongelea zoezi la kusaini mikataba baina ya maafisa watendaji wa kata na maafisa watendaji wa mitaa na vijiji, alilitaja zoezi hilo kuwa linalenga kufikia dhamira moja ya kukabiliana na tatizo la lishe katika Halmashauri hiyo. “Katibu Tawala Mkoa amesaini mkataba na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji juu ya utekelezaji wa masuala ya lishe. Mkurugenzi pia amesaini mkataba na maafisa watendaji wa Kata, ambao nanyi mtasaini mtakaba na maafisa watendaji wa Mitaa na Vijiji” alisema Ngowi.
Ngowi alisema kuwa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt John Magufuli inataka matokeo ya kazi. “Serikali hii inataka kumfanya mtumishi apimwe kulingana na matokeo ya kazi. Lazima tutumie vizuri mishahara tunayolipwa kwa kufanya kazi na kutoa matokeo chanya” alisisitiza Ngowi. Aliwataka kutekeleza matakwa ya mkataba wa lishe vizuri na kuwataka kutoa taarifa mapema watakapokutana na changamoto zinazokwakwamisha kufikia malengo wakati wa utekelezaji.
Kwa upande wake Afisa Lishe wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Semeni Eva Juma alisme kuwa hali mbaya ya utapiamlo inasababishwa na ulishaji duni, maradhi ya mara kwa mara na huduma hafifu za malezi na makuzi ya awali ya watoto wadogo. “Utapiamlo unachangia maradhi, vifo na uchelewaji wa ukuaji wa mwili na maendeleo ya akili kwa watoto” alisema Juma.
Akiongelea malengo ya mkataba baina ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji na watendaji wa Kata, alisema kuwa lengo kubwa ni kufanikisha suala la kuboresha hali ya lishe na kupunguza athari za utapiamlo katika jamii. Malengo mengine aliyataja kuwa ni kuhakikisha jamii kupitia uongozi wa Kata inashiriki ipasavyo katika kupanga, kutekeleza na kufuatilia maendeleo ya utekelezaji wa mpango wa Halmashauri na afua za lishe. Aidha, aliwataarifu kuwa maafisa watendaji hao wa kata watawajibika kuwasilisha taarifa za utendaji kazi kuhusiana na mkataba huo kwa robo mwaka, nusu mwaka na mwaka katika ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji.
Akiongelea tathmini ya mafunzo hayo, mshiriki ambaye pia ni Afisa Mtendaji Kata ya Chahwa, Monica Mongo alisema kuwa mafunzo yameamsha ari ya utendaji wao. ‘’Kwa kweli muelimishaji yupo vizuri mno. Binafsi nimemuelewa kwa asilimia 90. Hiyo asilimia 10 nitajiongeza ili kuweza kufanikisha hilo. Ushauri wangu haya ya leo yalikuwa ni mafunzo kwa lengo la kwenda kuelimisha jamii katika maeneo yetu. Kipindi kingine mafunzo kama haya yaratibiwe kwa wigo mpana ili tuwe na siku mbili au tatu. Siku hizo zitatupa urahisi wa kwenda kutekeleza. Changamoto kwenye Kata zetu ni kubwa mno usipoiva vizuri ni shida. Mwisho tunajiamini tutayafanyia kazi yote tuliyofundishwa’’ alisema Mongo
Mkataba baina ya Mkurugenzi na Watendaji wa Kata utakuwa kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia tarehe 1 Julai, 2019 hadi 30 Juni, 2021 na utakuwa ukipimwa kila baada ya miezi sita ya utekelezaji.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.