KAIMU Mkuu wa Idara ya Utawala na Utumishi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Innocent Kessy amewataka watendaji wa Kata kukabiliana na ujenzi holela katika Kata zao ili kufikia dhamira ya Jiji hilo kuwa Jiji lililopangiliwa kitaalam.
Kessy ametoa wito huo alipokuwa akifungua kikao kazi baina ya viongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma na watendaji wa Kata kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma leo.
Jiji la Dodoma linakuwa haraka katika sekta nyingi. “Kwa sasa katika Jiji la Dodoma kuna mfumuko mkubwa wa ujenzi, lakini ujenzi huo hauendani na mapato yatokanayo na vibali vya ujenzi. Kwa maana hiyo inaonesha kuwa ujenzi katika maeneo mengine unafanyika bila vibali rasmi vya ujenzi” amesema Kessy.
Aidha, aliwataka watendaji hao kwa kushirikiana na watendaji wa mitaa kusimamia na kudhibiti ujenzi holela. “Ujenzi holela unafanyika katika mitaa na kata zenu, hivyo mnawajibu wa kusimamia na kudhibiti ujenzi holela” amesisitiza Kessy.
Vilevile, Kessy aliwataka watendaji hao kuzingatia maelekezo yatakayotolewa na wakuu wa Idara mbalimbali katika kuboresha utendaji kazi wao na kuiwezesha Halmashauri kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi.
Akiongelea upitishaji wa barua unaofanywa na watendaji wa kata kwenda Halmashauri, amewataka watendaji hao wanapopitisha barua kutoa na maoni yao juu ya utekelezaji wa jambo husika.
Kikao kazi hicho pamoja na mambo mengine kilijadili ukusanyaji mapato ya Halmashauri, mikopo ya vikundi vya wanawake, vijana na wenye ulemavu, kilimo, mazingira na mifugo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.