MKURUGENZI wa huduma za tiba Wizara ya Afya Prof. Paschal Ruggajo amesema, jumla ya Watoa huduma za Afya 3000 wa mikoa 26 kupewa mafunzo ya utoaji huduma za kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza ili kuwakinga wananchi ifikapo Desemba 2023.
Prof. Ruggajo amesema hayo leo Oktoba 24, 2022 Jijini Dodoma wakati akifungua mafunzo ya kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza kwa Watoa huduma za Afya, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali katika mapambano dhidi ya magonjwa hayo.
"Moja kati ya mikakati iliyopo ni kuimarisha huduma za msingi kuwapa mafunzo Watoa huduma za Afya juu ya utoaji wa huduma za kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza. Watoa huduma 3000 kufikiwa kutoka Mikoa 26", Amesema Ruggajo
Amesema, moja kati ya mikakati iliyopo ni kuimarisha huduma za msingi kwa kuvijengea uwezo vituo vya Afya 600 kwa kuwapa mafunzo Watoa huduma za Afya juu ya utoaji wa huduma za kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza utaosaidia katika kuwahudumia wananchi.
Sambamba na hilo, Prof. Ruggajo amesema, Mafunzo haya yanayofanyika sasa ni awamu ya IV, hadi kufikia 28 Oktoba 2022, jumla ya watoa huduma 400 kutoka katika vituo vya Afya 94 vya mikoa minne ambayo ni Dodoma, Lindi,Songwe na Kigoma watajengewa uwezo katika kutoa huduma za magonjwa yasioambukiza.
Aidha, Prof. Ruggajo amesema, mafunzo haya kwa Watoa huduma yatakuwa msaada mkubwa kwa jamii kwani watatumika katika kutoa elimu ikiwemo kuishi mtindo wa Maisha unaofaa kama kuacha tabia bwete na kufanya mazoezi, kuzingatia ulaji unaofaa, kuepuka matumizi ya pombe yaliyopita kiasi na kuepuka matumizi ya tumbaku.
Naye, Mkurugenzi Msaidizi magonjwa yasiyoambukiza Dkt. James Kihologwe amesema, utafiti uliofanyika 2020 wa kuangalia utayari wa kutoa huduma ulionesha vituo vya kutolea afya nchini vipo tayari kutoa huduma za magonjwa yasioambukiza kwa chini ya asilimia 50%, tofauti na huduma nyingine kama huduma ya mama na mtoto na huduma za UKIMWI ambazo zilikuwa zikotolewa kwa takribani asilimia 94.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.