KAMBI ya uchunguzi na matibabu ya Moyo kwa watoto imeanza leo Septemba 26 katika hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma ikiwashirikisha madaktari Bingwa bobezi wa Moyo wa Hospitali hiyo na wenzao kutoka shirika la One Heart Faundation la nchini Marekani.
Watoto 13 wanatarajiwa kufanyiwa matibabu ya moyo katika kambi hiyo maalumu kati ya leo na Ijumaa. Dkt. Rehema Yona, Daktari bingwa wa Afya ya Mtoto amesema kuwa hadi kufikia asubuhi ya leo, watoto 11 wamelazwa kwa ajili ya maandalizi ya matibabu ya Moyo.
“Baadhi watafanyiwa upasuaji wa kufungua kifua na wengine watafanyiwa upasuaji wa matundu madogo kupitia njia ya mshipa wa paja katika maabara yetu maalumu ya Uchunguzi na Matibau ya Moyo (Cath-Lab)” Amesema Dkt. Yona.
Watoto hao 13 wanaotarajiwa kupatiwa matibabu hayo walikutwa na matundu kwenye Moyo, matatizo katika mishipa na milango ya Moyo.
Jopo la watu 22 likihusisha madaktari bingwa bobezi, wauguzi na wataalmu mbalimbali wa Moyo kutoka nchini Marekani tayari wamekwishawasili na kuungana na wenzao wa Hospitali ya Benjamin Mkapa na Hospitali ya Rufaa ya Bugando katika kambi hiyo maalumu ya siku 5 tayari kufanya uchunguzi na matibabu ya Moyo kwa watoto kuanzia leo Septemba 26 hadi 30.
Kwa siku zote tano, kambi hiyo itaendelea kufanya uchunguzi wa magonjwa ya Moyo ya watoto hospitalini hapo ili kuwaweka katika mpango wa matibabu katika kambi itakayofuata.
Chanzo: Ukurasa rasmi wa BMH (Instagram)
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.