Na. Asteria Frank, DODOMA
Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Rachel Balisidya amewataka wazazi kuwalinda watoto wao dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia na kuhakikisha wanaweza kutimiza ndoto na malengo yao kwa kuzuia madhara yanayoweza kuwaharibia maisha kisaikolojia.
Wito huo aliutoa leo alipomuwakilisha Katibu Tawala wa Wilaya ya Dodoma kwenye Tamasha la Tanzania Shiriki Malezi Endelevu Kupinga Ukatili (TASHMEKU) katika Shule ya Sekondari Dodoma Makulu kwa lengo la kupinga ukatili wa kijinsia kwa watoto.
Balisidya alisema kuwa Wilaya ya Dodoma bila ukatili inawezekana. Alisema kuwa ipo changamoto ya ukatili kwa watoto na asilimia kubwa ya ukatili inaanzia nyumbani kupitia baba, mama, mjomba, mwalimu na wale wanaowazunguka na kuwaharibu watoto kisaikolojia kwa kuwatesa, kubakwa na kuwanyima haki zao za msingi. “Tuhakikishe katika kipindi hiki cha likizo tuendelee kutoa elimu kwa wazazi ili kulinda usalama wa watoto na kuwalinda na wale watu wanaofanya ukatili juu yao. Wazazi wanatakiwa kuhakikisha wanakuwa karibu na watoto wao ili kuwalinda na waweze kuwaambia ukweli kuhusu jamii ilivyo kwa sasa” alisema Balisidya.
Kaimu Afisa Mtendaji wa Kata ya Dodoma Makulu, Method Karoly aliwaomba wazazi kupinga ndoa za utotoni kwa sababu wanawaumiza watoto wanaozaliwa kwa kutopata malezi mazuri kutokana na wazazi wenyewe kuwa wadogo na wapo chini ya umri wa miaka 18 na kukosa malezi bora. Alisema kuwa ndoa za utotoni pia ni ukatili wa kijinsia na kuliko waolewe ni bora watoto wapewe elimu ili iweze kujisaidia wao wenyewe. “Watoto wanaoingia kwenye ndoa za utotoni wanakutana na mambo mengi sana ya ajabu na hivyo, akili zao zinaharibika mpaka wanakuwa wanashindwa hata kuwalea watoto wao na wanachukulia ndoa za utotoni ni za kawaida na kuwafanyia hivyo kizazi chao pia”. alisema Karoly.
Nae, Wanafunzi wa Shahada ya Sheria Mwaka wa Pili Chuo Kikuu cha Dodoma, Jamal Mwasanjala alisema madhara wanayopata watoto wanaofanyiwa ukatili ni pamoja na kupata tatizo la afya ya akili, huzuni na kushidwa kuongea mambo ya msingi akiwa na watu. “Asilimia kubwa watoto wengi wanakuwa na tatizo la afya ya akili kwasababu malezi waliyopewa ni malezi magumu unaweza kushangaa mtoto anakaa na mzazi wake lakini anashindwa kuongea hata na mzazi kuhusu tatizo au madhara na chanzo cha unyanyasaji mtoto aliopitia” alisema Mwasanjala.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.