WATOTO waishio katika mazingira magumu kwenye Jiji la Dodoma wamemueleza Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, (Mb), madhila wanayokumbana nayo katika mitaa wanayoishi huku wakiiomba Serikali iweze kuwanusuru na maisha hayo kwa kuwa siyo kusudi lao kuishi hivyo.
Hayo yamejiri jana Januari, 17, 2022 Waziri huyo alipoongoza jopo la wataalamu wa Wizara hiyo, Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwenda mitaani wanakoishi watoto hao kwa ajili ya kuzungumza nao na kujifunza toka kwao jinsi gani Serikali inaweza kuwabadilishia maisha yao yawe na ustawi zaidi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti watoto hao walioweza kufikiwa, walisimulia madhila na changamoto wanazopitia wakiwa katika mitaa mbalimbali ya Jiji la DODOMA.
“Mhe. Waziri, sisi watoto tuishio katika mazingira ya mitaani tunapitia madhila mengi sana, tunalazimika kutumia vilevi, kujifunza mambo mengi mabaya pia tunafanyiwa mambo mabaya na tunalazimika kuwa watu wasio wema ili tuishi na matokeo yake tunabaguliwa na kutengwa na jamii” alisema mmoja wa watoto ambaye jina lake limehifadhiwa kwa sababu za kimaadili.
Vilevile, mtoto huyo, alisema wapo baadhi yao wamekuwa wakipitia ukatili wa kupigwa na wenzao wanaowazidi umri, wapo wanaofanyiwa ukatili wa kingono na kuambukizwa magonjwa na kupata maradhi ambayo mwisho wa siku yameondoa uhai kwenye umri mdogo.
Waziri Dkt Gwajima, akizungumza na Watoto hao, aliwaambia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuboresha ustawi wa watoto na ameunda Wizara mpya ambayo pamoja na mambo mengine itasimamia maendeleo na ustawi wa makundi maalumu ikiwemo watoto kwa ujumla wake.
Hivyo, ziara hiyo ya kujifunza huu ni mwanzo wa safari ya kuwaondoa watoto wanaoishi mitaani, wakaishi maisha salama na yenye ustawi hivyo wananchi na watendaji toeni ushirikiano kwani ufumbuzi wa jambo hili utatokana na wanajamii wenyewe.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Zainab Chaula, alisema tayari ameanza kuratibu ushirikiano na makatibu wakuu wa Wizara zingine ili watoe ushirikiano kwenye operesheni hii kubwa ya kuwarejesha watoto wa mitaani kwenye maisha yenye ustawi na atasimamia jambo hili kwa ushirikiano na wadau wengine wote.
Kwa upande wake Kaspar Kaspar Muya, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu amesema, ofisi hiyo iko tayari kuratibu ushirikishwaji wa wizara na Sekta zote ili jambo hili lifanikiwe kama ilivyokusudiwa kwenye Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA, 2017/18-2021/22) na ILANI ya Uchaguzi Mkuu CCM, 2020-2025.
Kama sehemu ya mpango wa haraka, Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu imeanza kuratibu kuwezesha watoto waishio kwenye mazingira magumu ya mitaani wanarejea kwenye maisha yenye ustawi ili wakiwa watu wazima waweze kuchangia maendeleo ya taifa kwa tija.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Fatma Mganga akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo amesema, Mkoa upo tayari kushirikiana na wadau wote kusimamia utekelezaji wa zoezi hilo kwa ufanisi.
Ziara hiyo imefanikisha kuwarejesha watoto 14 kwenye makao ya watoto na uratibu unaendelea mkoani Dodoma na utaendelea mikoa yote.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.