SERIKALI imezindua rasmi zoezi la kukabidhi kadi za bima ya Afya ya Jamii iliyoboreshwa (iCHF) katika mikoa yote 24 ya Tanzania Bara na Halmashauri 81 ambapo watoto 92, 926 ambao ni sawa na kaya 361, 530 watapatiwa kadi hizo zitakazowasaidia katika kupata matibabu kwenye hospitali mbalimbali.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Dkt. Festo Dugange amezindua rasmi zoezi la kukabidhi kadi hizo kitaifa katika hafla iliyofanyika katika eneo la Magufuli Square ndani ya Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo Jijini Dodoma ambapo amewapongeza wadau wote ikiwemo Serikali na Shirika lilsilo la kiserikali la PACT kupitia mradi wake wa USAID Kizazi Kipya ambalo ndiyo limegharamia bima hiyo kwa kutoa shilingi bilioni 4.6 ili kuwafikia walengwa hao kote nchini.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika Alhamisi Februari 11, 2021 Dkt. Dugange alitoa maagizo kwa Wakuu wa Mikoa kote nchini kusimamia zoezi hilo katika mikoa yao ili liwe na ufanisi na walengwa wote wakabidhiwe kadi zao za bima kama ilivyokusudiwa na Serikali na wadau wake.
Kwa upande wao wazazi na walezi wa watoto 20 waliokabidhiwa kazi zao kwa niaba ya watoto wenzao wameishukuru Serikali na Shirika la PACT kwa kuwapatia bima ya afya huku wakitoa wito kwa wananchi wengi zaidi kujiunga na bima hiyo kwani imekuwa kama mkombozi wa wananchi wa hasa wenye uchumi wa chini pale wanapokuwa katika changamoto ya maradhi.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya madiwani wa nchi nzima, Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii Halmashauri ya Jiji la Dodoma ambaye pia ni Diwani wa Kata Chahwa Mhe. Sospeter Mazengo (kushoto pichani juu) aliishukuru Serikali na Shirika la PACT kwa mradi huo alioutaja kama neema kubwa hasa kwa walengwa hao ambao kimsingi wana changamoto kubwa ya kumudu gharama za matibabu.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.