WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar Es Salaam, Bw. Jumanne Shauri pamoja na watumishi wengine tisa wa jiji hilo ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za Serikali ambazo ni zaidi ya shilingi bilioni 10 zilizokusanywa na hazikuwasilishwa benki kama sheria inavyoelekeza.
Agizo hilo linatokana na matokeo ya ukaguzi maalum kuhusu Mapato ya Ndani katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa mwaka wa fedha 2019/2020 hadi 2020/2021 uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG). Watumishi hao pia wamekabidhiwa kwa Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Dar Es Salaam kwa mahojiano juu ya tuhuma zinazowakabili.
Mheshimiwa Majaliwa ametoa taarifa hiyo leo (Jumatatu, Julai 11, 2022) wakati akizungumza na viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam, Wabunge, Madiwani pamoja na watumishi wa wilaya ya Ilala katika ukumbi wa Karimjee akiwa katika ziara yake ya kikazi Dar Es Salaam.
Mheshimiwa Majaliwa amesema mbali na Mkurugenzi huyo wa Halmashauri ya Jiji la Dar Es Salaam, watumishi wengine ni pamoja na Tulusubya Kamalamo (Mweka Hazina), James Bangu (Mhasibu Mapato), Abdallah Mlwale (Mtunza Fedha Mkuu) na Mohammed Khais (Mhasibu wa Masoko).
Amesema watumishi hao wanatuhumiwa kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo na hivyo kuisababishia Halmashauri hasara ya jumla ya kiasi cha shilingi 10,137,577,401 zilizokusanywa na mawakala na watumishi wa Halmashauri hiyo lakini hazikuingizwa benki.
Pia, Waziri Mkuu ametaja watumishi wengine wanaopaswa kuchukuliwa hatua kuwa ni Jesca Lugonzigwa (Afisa Hesabu), Josephine Sandewa (Afisa Hesabu), Tatu Mkangwa (Kibarua) na Felician Maro (Mhasibu Msaidizi) ambao wameisababishia halmashauri hasara ya shilingi 1,214,907,637.
Waziri Mkuu ametaja mawakala wanaodaiwa kufanya udanganyifu wa makusanyo ya mapato kwa kuchezea tarehe za PoS kwa kuzirudisha nyuma na hivyo makusanyo ya kiasi cha shilingi 131,356,400 kutoonekana kwenye taarifa za makusanyo. Mawakala hao ni Pick Trading Ltd na Workers General Supply.
“Ripoti ya CAG imebaini kuwa wataalamu wa Halmashauri waliohusika na upotevu wa mapato walikuwa wakiingilia moja kwa moja kati ya mfumo wa LGRCIS na benki na kuandika kwenye mfumo malipo ambayo hayakufika benki kwa lengo la kuficha ukweli wa kasoro na matumizi ya fedha kinyume cha sheria za fedha za umma. Pia wahasibu waliingiza kwenye mfumo kiasi ambacho hakikupelekwa benki kwa lengo la kupotosha taarifa halisi za makusanyo.”
Waziri Mkuu amesema Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amesisitiza kuwepo kwa umakini kwenye ukusanyaji na matumizi ya mapato ili kuiwezesha Serikali kuendelea kujenga miradi mingi zaidi kwa ajili ya maendeleo ya wananchi. “Ilala pamoja na kupata hati safi lakini ndani yake kuna mambo ambayo hayana tija.”
“Uko mwenendo wa kutengeneza udanganyifu katika ukusanyaji na matumizi ya mapato ya halmashauri, kuna wakati wanaamua kuzima kwa saa mbili hadi tatu mfumo kwa kisingizia cha mtandao na pamato yatakayopatikana kwa muda huo hayafuati taratibu kwani badala ya kuipeleka benki inatumika kwa visingizio mbalimbali kama kulipa vibarua.”
Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dar Es Salaam ufuatilie vyanzo vyote vya mapato vya halmashauri hiyo na pia waweke makadirio ambayo yatawawezesha kukusanya zaidi. Pia amewasisitiza waweke makadirio yatakayowawezesha kufanya kazi zaidi na kila muhusika ahakikishe anatekeleza majukumu yake ipasavyo.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Innocent Bashungwa, Katibu Mkuu wa TAMISEMI, Profesa Riziki Shemdoe, Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam, Amos Makala pamoja na maafisa wengine wa Serikali.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.