Kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka huu, Halmashauri ya Jiji la Dodoma imewaapisha watumishi 263 kuwa wasimamizi wasaidizi wa ngazi ya Kata na Mitaa ndani ya Wilaya ya Dodoma mjini na kuwapa maelekezo ya uchaguzi.
Wasimamizi hao wameapishwa na Hakimu Mkazi wa Dodoma Rachel Jacob Magoti mapema leo katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Umonga iliyopo Area A jijini hapa.
Aidha, Msimamizi wa Uchaguzi wa Jiji la Dodoma Dickson Kimaro alitoa maelekezo kuhusu tarehe ya uchaguzi utakapofanyika na majukumu ya wasimamizi hao wakati wa uchaguzi. "Tutafanya uchaguzi wa Serikali za Mitaa siku ya tarehe 24/11/2019 na sisi kama wasimamizi wa uchaguzi tunapaswa kufuata maadili ya utumishi wa umma kwa uzalendo na ufanisi wa hali ya juu".
Vile vile Afisa Uchaguzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Hidaya Maeda amewaomba watumishi hao kutunza kiapo chao, kuepukana na rushwa na kufanya kazi kwa uaminifu. "nawaomba jamani tujiepushe na rushwa ambazo zitakufanya ukiuke maadili ya kazi yako, tujitahidi tafadhari" alionya Maeda.
Aidha, Maeda aliwapitisha wajumbe kwenye Mwongozo wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2019. Mwongozo huo unafafanua shughuli zote za uchaguzi kuanzia maandalizi hadi upigaji kura utakapokamilika.
Watumishi hao waliokula kiapo cha utii na uaminifu walipata wasaa wa kuuliza maswali ili kupata uelewa zaidi wa majukumu yao ya kusimamia uchaguzi.
Vilevile, Afisa kutoka kitengo cha Uchaguzi Martin Tumaini alikuwakumbusha kuhusu kanuni ya 11 kuhusu uandikishaji wa wapiga kura.
Baada ya kipindi cha maswali na majibu kuisha, Msimamizi wa Uchaguzi alifunga warsha hiyo na kuwatakia utekelezaji mzuri wa majukumu yao kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba, 2019.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.