Na. Faraja Mbise, DODOMA
Maelfu ya watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma wajitokeza kwa wingi katika Uwanja wa Jamhuri kushiriki Bonanza la kuaga na kukaribisha mwaka mpya 2025.
Akizungumza wakati wa Bonanza hilo, Diwani wa Kata ya Mtumba, Edward Maboje, alisema kuwa, katika utumishi wake wa miaka kumi hajawahi kuona bonanza la namna hiyo kuwahi tokea na alitumia nafasi hiyo kumshukuru Mkurugenzi wa Jiji kwa kuwakutanisha watumishi wote kwa lengo la kuimarisha mahusiano bora katika utendaji kazi. “Mimi nina mwaka wa 10 katika udiwani, toka nimekuwa Diwani halijawahi kutokea bonanza kama hili. Nadhani niseme hili bila kuficha, kiongozi wa halmashauri kwa maana ya mkurugenzi, ana upeo mkubwa sana kwa watumishi wake” alisema Maboje.
Kuhusu masuala ya mahusiano mema katika utendaji na uboreshaji wa kazi, alisema, kukutanishwa kwa watumishi hao kunajenga msingi bora wa maelewano na mshikamano. Maboje alisema “bonanza hili linaonesha namna ambavyo Mkurugenzi ana mahusiano mazuri na watumishi anaowaongoza, kwa kufanya hiki kitu kinajenga msingi wa maelewano na mshikamano. Maana yake kama mtumishi anapoambiwa kuna majukumu fulani, atakuwa anakumbuka kuwa mimi nimeshafanyiwa kitu hiki kwamba mkurugenzi anatujali. Kwahiyo, ninataka kusema kuwa, hii hapa ni tija katika ufanisi wetu wa kazi na kufanya kazi kama timu”.
Aidha, alitoa wito kwa watumishi waliohudhuria Bonanza hilo kuendelea kudumisha mshikamano waliouonesha na kuufanyia kazi katika utoaji huduma kwa jamii. “Natoa wito kwa watumishi, mshikamano waliouonesha leo, uendelee na hata katika kutoa huduma kwa jamii na idara zote. Hili jambo la leo mkurugenzi na menejimenti yake wameonesha wema wao kwa kutujali watumishi wa ngazi zote. Kwahiyo, nawaomba watumishi na madiwani wenzangu tufanye kazi kwa mshikamano na kwa ushirikiano mkubwa ili tuiinue halmashauri yetu na izidi kupanda” alitoa wito Maboje.
Kwa upande wake Mtendaji wa Kata ya Mtumba, Hassan Kadoke, alipongeza bonanza hilo kwasababu limewakutanisha watumishi mbalimbali na kufahamiana pia limeshirikisha michezo mbalimbali iliyolenga kuimarisha na kuboresha afya. “Siku ya leo imekuwa nzuri kwetu sisi watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, kupitia maandalizi mazuri aliyoyafanya Mkurugenzi wa Jiji kuandaa bonanza la kutukutanisha sisi watumishi wa serikali. Kikubwa katika hili Bonanza tunachofurahi ni kwamba, limekutanisha watumishi wote na idara mbalimbali, kwanza, kuja kufurahi na pili kufahamiana kwasababu kuna baadhi ya idara hatufahamiani, watumishi kwa watumishi hatufahamiani. Kwahiyo, limetukusanya watumishi wote na tumeweza kufahamiana” alipongeza Kadoke.
Nae, Afisa Michezo wa Jiji la Dodoma, Peter Ititi, alishiriki mashindano ya Mchezo wa Drafti na kuibuka kidedea katika fainali za mchezo huo ambapo awamu ya kwanza aliibuka mshindi. “Nimejipanga, nimejifua wiki nzima nikijiandaa kushinda Mchezo wa Drafti na mpaka sasa mchezo wangu wa kwanza nimeshinda. Kwahiyo, ninasubiri mshindi wa mchezo wa pili ili nicheze nae. Nina hakika kombe hili ni la kwangu na lazima niwe mshindi wa kwanza kwa vyovyote vile” alisema Ititi.
Bonanza lilifana kwa kuanza na mbio za taratibu ‘jogging’ na kufuatia na michezo na burudani mbalimbali zilizopendezesha tamasha hilo kama mpira wa miguu, netiboli, kuvuta kamba, mchezo wa bao, drafti, kukimbiza kuku na burudani na muziki wa asili, utenzi na kizazi kipya kutoka kwa wasanii nguli jijini hapo. Bonanza hilo lilikuwa na lengo la kuukaribisha Mwaka 2025 na kuwakaribisha watumishi wote waliohamia Halmashauri ya Jiji la Dodoma na kuwaaga wastaafu wote chini ya kaulimbiu isemayo “Halmashauri ya Jiji la Dodoma 2025, Ushirikiano na Umoja Wetu Ndio Nyenzo ya Huduma Bora”.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.