WATUMISHI wa umma katika Halmashauri ya jiji la Dodoma wameshauriwa kushiriki kikamilifu katika zoezi la usafi wa mazingira katika maeneo yao na maeneo yanayopangwa na serikali kufanyiwa usafi ili wawe mfano bora kwa jamii.
Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa Idara ya Usafi wa Mazingira na Udhibiti wa Taka ngumu katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dickson Kimaro alipokuwa akiongea na waandishi wa habari baada ya kumalizika kwa zoezi la usafi wa mazingira lililoambatana na maadhimisho ya wiki ya utumishi wa umma na kufanyika katika Kata ya Viwandani Jijini Dodoma leo.
Kimaro alisema kuwa zoezi la usafi wa mazingira ni zoezi la wananchi wote, watumishi wa umma wakiwemo, hivyo wanatakiwa kushiriki kikamilifu. Watumishi wa umma ni kielelezo katika jamii inayowazunguka katika kusimamia na kutekeleza maelekezo ya serikali, aliongeza. Aidha, alisema kuwa watumishi hao kujitokeza kushiriki katika usafi wa mazingira ni njia ya kujiweka karibu na wananchi na taasisi wanazofanyia kazi kufahamika vizuri kwa wananchi.
Akiongelea tathmini ya zoezi la usafi wa mazingira katika Kata ya Viwandani eneo la Chako ni chako na maeneo ya jirani, Kimaro alisema kuwa wananchi wamejitokeza kwa wingi kufanya usafi katika mitaro na maeneo ya wazi. “Changamoto kubwa katika Kata ya Viwandani eneo maarufu la Chako ni chako, wafanyabiashara wanapofanya biashara usiku hawafanyi usafi katika maeneo yao na asubuhi hawaji kufanya usafi na kusababisha kero kwa watumiaji wa maeneo hayo na mazingira kwa ujumla. Mitaro tumekuta ni michafu na wahusika wanaenda kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria ndogo za halmashauri ya jiji” alisema Kimaro.
Kwa upande wake, Afisa utumishi katika Halmashauri ya jiji la Dodoma, Joyce Kisege aliyeshiriki zoezi hilo alisema kuwa watumishi wa umma wanawajibu wa kipekee kushiriki katika usafi wa mazingira. “Watumishi wa umma ni sehemu ya jamii hivyo huwezi kuwatenganisha na jamii inayowazunguka. Kwa kushiriki kwao katika masuala ya usafi wa mazingira kuna halalisha usehemu yao katika jamii na kuwaweka karibu na wananchi. Hivyo, huduma wanazotoa zinaweza kuanzia hukohuko katika jamii kabla ya kufika ofisini” alisema Kisege. Aidha, aliongeza kuwa watumishi hao ni sehemu ya uhamasishaji jamii kwa ujumla. Wananchi wanapoona watumishi wa umma wanashiri katika zoezi la usafi wanahamasika kufanya usafi, aliongeza Kisege.
Mkazi wa kaya ya viwandani, juma Abdallah alisema kuwa ushiriki wa watumishi wa umma unaondoa tofauti kati ya watumishi hao na jamii inayowazunguka.
Halmashauri ya Jiji la Dodoma inatekeleza zoezi la usafi kitaifa kila wiki ya mwisho wa mwezi na kufuatia agizo la mkuu wa mkoa wa Dodoma kuwa zoezi la usafi wa mazingira lifanyike kila siku ya jumamosi limekuwa likitekelezwa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.