WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amewataka Watumishi wa Umma kutoa huduma bora kwa wananchi huku akizitaka Taasisi zote za Umma kuhuisha Mikataba ya Huduma kwa Mteja kwani ni nyenzo na kiungo muhimu katika kuboresha utendaji kazi kati ya Serikali na Wananchi inaowahudumia.
Ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na watumishi mbalimbali wa Serikali pamoja na wananchi walioshiriki kwenye Uzinduzi wa Mikataba ya Huduma kwa Mteja ya Taasisi za Umma katika Kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma ambayo kitaifa yamefanyika katika Viwanja vya Nyerere Square Jijini Dodoma.
Mhe. Simbachawene amewataka Watumishi hao kutambua kuwa wanapotoa huduma bora kwa wananchi wanamuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa akisisitiza suala hilo mara kwa mara.Kufuatia hatua hiyo, amezitaka Taasisi za Umma kuzingatia Mikataba ya Huduma kwa Mteja katika utoaji wa huduma kwa wananchi ili haki na wajibu wa pande zote mbili utendeke kwa watoa huduma na wapokea huduma ambao ndio wateja.
Ameongeza kuwa Ofisi yake ina wajibu wa kusimamia mifumo na viwango vya utendaji kazi Serikalini kwa lengo la kuongeza uwajibikaji na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na moja ya mifumo na viwango vya Utendaji Kazi huo ni Mkataba wa Huduma kwa Mteja.
Awali, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Juma Mkomi amesema uzinduzi wa Mikataba ya Huduma kwa Mteja ni moja ya hatua muhimu ya kuboresha huduma bora kwa wananchi ambapo amesema jumla ya Mikataba ya Huduma kwa Mteja 34 ya Taasisi za Umma imeweza kuzinduliwa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.