Na. Faraja Mbise, DODOMA
Watumishi mbalimbali wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma wametakiwa kufanya kazi kwa mshikamano katika kutoa huduma zao kwa jamii ili kuweza kuiinua halmashari izidi kupanda katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Hayo yalisemwa na Diwani wa Kata ya Mtumba, Edward Maboje, alipokuwa akitoa wito katika Bonanza la Watumishi lililofanyika tarehe 25 Januari, 2025 katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
“Mshikamano uliooneshwa leo uendelee hata katika kutoa huduma kwa jamii kwa ngazi zote. Hili jambo la leo, mkurugenzi na timu yake wameonesha jambo la kutujali watu wa ngazi zote. Kwahiyo, na mimi ninawaomba sasa, watumishi na sisi madiwani tufanye kazi kwa mshikamano na kwa ushirikiano mkubwa ili tuiinue halmshauri yetu izidi kupanda. Mimi nimesema hili ni jambo jipya kwangu na mimi ni mtu mzima, ni jambo jipya. Pia, Dodoma hapa ni nyumbani, napafahamu vizuri na wakurugenzi wanapita wengi lakini hiki kitu kimenigusa na ninawaomba watumishi wa Halmashauri ya Jiji tufanye kazi kwa mshikamano” alisema Maboje.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Makole, Omary Omary, alitoa pongezi kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kuona kuna uhitaji mkubwa wa kuandaa Bonanza la Watumishi ambalo linakutanisha watumishi wote wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma ili waweze kufahamiana na kufurahi pamoja. “Nampongeza Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma kwa kuweza kutambua na kuona namna ya kuandaa bonanza zuri kama hili kwa ajili ya watumishi pamoja na viongozi mbalimbali ambao wanatoka Jiji la Dodoma. Sambamba na hilo, katika uwanja huu wa Jamhuri umefurika na umejaa viongozi wengi wa kutosha na kila kiongozi na mtumishi wa jiji anafurahia bonanza kwasababu kuna michezo mbalimbali inaendelea hapa. Kwahiyo, nimpongeze kwa kuweza kufanya jambo zuri kama hili” alipongeza Omary.
Nae, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Ihumwa, Mwl. Daudi Mwakalinga, alisema kuwa, kufanya tathmini ya kukutana mara moja kwa mwaka inaleta picha nzuri na kuwaweka pamoja watumishi na inazidisha umoja na mshikamano. “Tamasha limekuwa zuri na mpaka sasahivi ninavyozungumza watu wengi wamefurahia tamasha hili. Kukutana watumishi mara moja kwa mwaka na kufanya tathmini ya mambo yote tuliyoyafanya kwa furaha, tukafanya michezo mbalimbali hii inatuweka pamoja watumishi na inatufanya tuonekane kwamba tunapendana na tunajenga nyumba moja. Nia kuu ya watumishi ni kuhakikisha jiji linasonga mbele na maendeleo ya taifa yanapatikana kwa umoja wetu kwa kila sekta” alisema Mwl. Mwakalinga.
Aidha, alishauri kuwa, Bonanza hilo lisiwe la mwisho bali likawe mwanzo wa mabonanza mengine katika Jiji la Dodoma ili kuweza kuimarisha mahusiano mazuri baina ya watumishi wote wa Halmashauri ya Jji la Dodoma.
Hata hivyo, Afisa Utamaduni katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Desdery Kuzenza, aliwashukuru washiriki wote waliohudhuria Bonanza la Watumishi kwa kuwakumbusha kuwa, bonanza hilo ilikuwa ni ishara ya kufungua Mwaka Mpya 2025 na kuwasisitiza kutekeleza dhima na dira ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kutoa huduma iliyo bora kwa wananchi.
Kuzenza alisema “nitumie fursa hii kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma na Menejimenti kwa ujumla kuwashukuru washiriki wote wa Bonanza. Bonanza hili ni ishara ya kuanza mwaka mpya katika maono ambayo yamejielekeza kupeleka huduma kwa wananchi na wakazi wa Dodoma sambamba na kutekeleza dira na dhima za Halmashauri ya Jiji la Dodoma ili kuhakikisha kwamba tunatoa huduma bora, za uhakika na zinazokidhi malengo ya walengwa wetu ambao ni wananchi”.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.