Watumishi kutoka Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa wameshiriki mafunzo ya Utunzaji wa Nyaraka na Kumbukumbu Serikalini Jijini Dodoma.
Mafunzo hayo yamelenga kuongeza ufanisi na umahiri katika uandikishaji, utunzaji pamoja na utoaji wa nyaraka mbalimbali na kumbukumbu Serikalini.
Akizungumza kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu (TAMISEMI) Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Utawala Usimamizi na Rasilimali Watu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Bw. Marko Masaya ametoa wito kwa watumishi hao kuzingatia taratibu na kanuni za uandikishaji, utunzaji na utoaji wa nyaraka Serikalini kama ilivoainishwa katika miongozo mbalimbali.
Ameongeza kuwa mafunzo hayo ni fursa pekee katika kuleta maboresho na kuongeza ufanisi katika utendaji kazi, hivyo kila mmoja ana wajibu wa kuongeza umahiri katika utendaji kazi kupitia mafunzo hayo.
"Mafunzo haya yana tija katika utendaji kazi wetu, hivyo basi yale tuliyokumbushana leo tukayafanyie kazi na kuboresha pale palipopwaya", alisema Masaya
Kwa upande wake mwezeshaji Norbert Cyrille kutoka Ofisi ya Rais, Utumishi Idara ya kumbukumbu na Nyaraka za Taifa ametoa wito kwa maafisa hao kufuata miongozo iliyowekwa na kuacha kufanya kazi kwa mazoea katika utunzaji wa nyaraka na kumbukumbu Serikalini.
Mafunzo hayo ni zoezi endelevu ambapo awali yalitolewa kwa uongozi na menejimenti pamoja na maafisa kutoka idara mbalimbali Ofisi ya Rais- TAMISEMI.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.