Watumishi wa umma na binafsi wametakiwa kuwa makini na chochote wanachofanya mtandaoni ili kujilinda na changamoto za uhalifu wa mtandao ambapo katika zama hizi za kidijiti taarifa binafsi au za taasisi zimegeuka kuwa malighafi muhimu kwa wahalifu wa mtandao.
Hayo yamezungumzwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Usalama Mtandao wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Stephen Wangwe wakati akitoa elimu ya usalama mtandao kwa Menejimenti ya Chuo cha Ufundi cha Arusha, Oktoba 17, 2022, jijini Arusha.
Mhandisi Wangwe amesema kuwa suala la usalama mtandao ni changamoto ya kidunia ambapo takwimu zinaonesha kila siku majaribio milioni 156 ya uhalifu kwa njia ya barua pepe au tovuti hutokea na majaribio milioni 16 hufanikiwa.
Ameongeza kuwa Serikali kupitia Wizara hiyo imeendelea kuimarisha usalama wa mtandao kwa kujenga mazingira wezeshi na mifumo imara ya kusimamia sera, sheria, kanuni na miongozo ya usalama wa mtandao pamoja na kutoa elimu kwa makundi yote katika jamii ili kupunguza mianya ya uhalifu wa mtandaoni.
“Usalama wa mtandao huanza na mtu binafsi, pamoja na juhudi nyingi zinazofanywa na Serikali, bado kila mtu analo jukumu la kuchukua tahadhari na kujilinda na uhalifu unaofanywa kwa njia ya mtandao”, Amesema Wangwe
Naye Mtaalamu wa Masuala ya Usalama Mtandao na Uchunguzi wa Kidijiti wa African ICT Alliance (AfICTA) kutoka Tanzania, Bw. Yusuph Kileo amesema kuwa, namba ya siri imara na madhubuti ni kitu cha kwanza na cha msingi za kujilinda na uhalifu wa mtandao lakini pia umakini na kuchukua tahadhari kutawaepusha watumiaji kuwa wahanga wa uhalifu wa mtandao.
Katika hatua nyingine, Mhandisi Wangwe amewataka wanafunzi wa Chuo cha Uhasibu cha Arusha (IAA) kutafakari mara mbili kabla ya kuweka chochote mtandaoni ili kujiepusha na matukio ya udhalilishaji na utapeli ambayo yanaweza kuathiri maisha yao ya baadae.
Akijibu maswali mbalimbali ya wanafunzi chuoni hap oleo oktoba 17, Mhandisi Wangwe ametolea ufafanuzi masuala kadhaa ikiwa ni pamoja na huduma ya bure ya kutafuta simu iliyoibiwa na umakini wa Serikali wa kujiridhisha kabla ya kuzifungia namba za simu zilizoripotiwa kufanya uhalifu kupitia namba 15040.
Mapokeo ya Elimu ya Usalama mtandao kwa Menejimenti ya Chuo cha Ufundi cha Arusha na wanafunzi wa Chuo cha IAA yamekuwa ni mapokeo chanya ambapo kwa nyakati tofauti wamekiri kuwa elimu iliyotolea imewafungua katika maeneo mengi sana na matamanio yao ni Wizara kuendelea kutoa mafunzo haya mara kwa mara na kuyafikia makundi yote ya kijamii.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.