UJUMBE wa watu sita wakiwakilisha Kampuni saba kutoka nchini Uturuki pamoja na Maofisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje wametembelea Jiji la Dodoma na kufanya kikao cha pamoja na wataalamu wa Jiji kwa lengo la kujua na kupata maeneo ya kufanya uwekezaji.
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi ameuelezea ujumbe huo kuwa Ofisi yake imeandaa mazingira rafiki kwa wawekezaji na wapo tayari kuwapokea na kuwapa ushirikiano wa kutosha wakati wowote.
“Tuna eneo maalum la ukanda wa uwekezaji la Njedengwa lakini pia katika mpango kabambe wa Jiji la Dodoma kuna maeneo mengi yatakayokuwa mahususi kwa ajili ya uwekezaji” alisema.
Miongoni mwa mambo ya msingi waliyotaka kufahamu wadau hao wa maendeleo ni namna Serikali ya Mkoa wa Dodoma hususani Jiji la Dodoma lilivyojipanga kuhakikisha uwepo wa miundombinu muhimu kama Barabara na nishati kama umeme na maji ilivyo sasa na mipango ya baadaye, kama nyenzo muhimu katika uwekezaji.
Baada ya maelezo ya Mkurugenzi wa Jiji Kunambi, na wataalam kutoka TANESCO na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA), wawekezaji hao wameonyesha kuvutiwa kuwekeza katika sekta za Hoteli, Maduka makubwa ya Biashara (Shopping Malls), Madini, uwekezaji katika Elimu, Kilimo na Viwanda.
Miongoni mwa maeneo yaliyowavutia wageni hao kutoka Uturuki ni pamoja na eneo maalumu la Uwekezaji Njedengwa, Mji wa Serikali utakaojengwa katika Kata ya Mtumba, Chuo Kikuu cha Dodoma, Jiografia, pamoja na hali ya hewa ya Mkoa wa Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.