WAUGUZI na Wakunga nchini wametakiwa kutoa huduma kwa kuzingatia miongozo iliyopo wakati wakitoa huduma kwa weledi ili kufikia malengo na matumaini ya wateja kwa ajili ya ustawi wa Taifa.
Rai hiyo imetolewa jana na Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto - Idara Kuu ya Afya Bwana Edward Mbanga wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha kuwajengea uwezo wa kusimamia maadili na utendaji kazi wauguzi wakuu wa wilaya kinachofanyika jijini Dodoma.
"Ili kuhakikisha Wananchi wanapata huduma bora, na waendelee kujenga uchumi, sisi tuliopo hapa, tunawajibu mkubwa sana wa kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais anazofanya, kwasababu hata kama Serikali itafanikiwa kujenga majengo ya nyota tano kwenye kila kituo cha kutolea huduma za Afya, kama hatutakuwa na Watumishi wenye moyo na wanaofanya kazi kwa kujitoa hayo majengo hayatasaidia kuokoa uhai wa Watanzania" alisema Kaimu Katibu Mkuu Wazara ya Afya - Idara Kuu Afya Bw. Edward Mbanga.
Bwana Mbanga amesema kuwa wauguzi na wakunga ndio watendaji wakuu katika vituo vya afya kwenye ngazi ya jamii hadi Taifa hivyo uwajibikaji mzuri na utawala bora utaboresha utendaji, hali itakayo saidia kufikia malengo mbalimbali waliyojiwekea katika ngazi zote.
"Viongozi mnatakiwa kuwa wabunifu, wachapa kazi, wenye nidhamu na mfano bora wa kuigwa katika utekelezaji wa majukumu yenu, kwahiyo ni lazima msimamie utoaji wa huduma ulio mzuri na wenye heshima na utu", alisema.
Aidha, Kaimu Katibu Mkuu huyo aliwakumbusha washiriki hao kuwa, suala la huduma za uuguzi na ukunga ni suala la ubinadamu zaidi na kuvaa viatu vya wagojwa wao.
"Hakuna aliyegongwa muhuri wa kuugua au kuwa mgonjwa akalazwa, sisi sote ni wagonjwa watarajiwa kwahiyo kama ambavyo sisi tungependa kuuguzwa vizuri, kujibiwa kwa kauli nzuri basi tuhakikishe tunasimamia maadili ya kazi" alisisitiza Mbanga.
Hata hivyo alisema kuwa Serikali inawahakikishia itaendelea kufanya kazi pamoja na wauguzi kwa kutoa miongozo thabiti na kuhakikisha upatikanaji wa nyenzo muhimu katika hospitali na vituo vya kutolea huduma ya afya na kuboresha mazingira ya kazi yaliyo bora na salama.
Aliendelea kusema kuwa, hivi karibuni kumekuwa na malalamiko mbalimbali ya kiutendaji na kitaaluma kutoka kwa wateja wanaofika kupata huduma za afya na hivyo kuleta taswila mbaya kwa taaluma yao na kuonyesha hakuna usimamizi mazuri wa utoaji huduma za uuguzi na ukunga.
"Tungependa wateja wetu watoe sifa nzuri badala ya malalamiko hivyo kikao hiki mje na mipango ya kuondokana na malalamiko kwani taaluma yenu ni zaidi ya taaluma" alisema Mbanga.
Chanzo: wizara_afyatz (instagram)
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.