Na. Theresia Nkwanga, UHURU
WAZAZI wa Kata ya Uhuru wametakiwa kulipa kipaumbele swala la malezi kwa watoto na kujenga utamaduni wa kuzungumza nao ili kuwalinda dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Kauli hiyo ilitolewa na Diwani wa viti maalum wa Jiji la Dodoma, Janeth Kusaduka alipokuwa akiongea na wananchi wa Kata ya Uhuru pamoja na wanafunzi wa Shule ya Msingi Uhuru iliyopo Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Kusaduka alisema kuwa wazazi wanatakiwa kutenga muda wa kuzungumza na watoto wao ili kusikiliza changamoto zinazowakabili, pia kupunguza ‘ubusy’ wakutafuta pesa na kuelekeza nguvu zao katika kulea watoto. “Wazazi siku hizi tupo ‘busy’ sana, asubuhi tunaenda kutafuta riziki hatuna muda na watoto tumewaachia walimu malezi ya watoto wetu. Watoto wanapitia changamoto nyingi sana, vijana wengi wanawadangaya watoto wetu kwa vitu vidogovidogo kama pipi na biskuti na kuwafanyia vitendo vya ukatili wa kijinsia. Wakati umefika sasa wazazi tuchukue nafasi zetu tuwalinde watoto wetu. Wazazi tutenge muda wakuzungumza nao kama rafiki zetu ili wawe huru kutuelezea changamoto zao” alisema Kusaduka.
Aidha, aliwaomba watoto kuvunja ukimya pindi wanapofanyiwa vitendo vya ukatili wa aina yoyote ile, kuripoti kwa watu wao wakaribu ili wahusika wafikishwe kwenye mikono ya sheria na kupewa adhabu stahiki. “Watoto msiogope chochote acheni kuficha siri mnavyowaficha wahalifu mnalea maradhi. Ukiona mtu anakugusa sehemu za mwili wako au anakubusu hivyo ni viashiria vya kufanyiwa vitendo vya ukatili msivifumbie macho, toa taarifa kwa walimu, wazazi au nenda Polisi usisubiri hadi ufanyiwe ukatili ndio utoe taarifa” alisema Kusaduka.
Kusaduka aliwashauri kina mama kuacha kulinda ndoa zilizojaa manyanyaso na ukatili. Aliwataka kupaza sauti pindi wanapofanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa kuwashtaki waume zao wanaoshiriki vitendo hivyo kwenye madawati ya jinsia, ili waweze kutokomeza matendo ya ukatili wa kijinsia katika ngazi ya familia.
“Kina mama vipigo wanapokea sana ila wanashindwa kushtaki kwa kisingizio cha hatuwezi kulea watoto wenyewe, mwisho wa siku wanaishia kupoteza maisha kwa vipigo na kuwaacha watoto yatima. Ndugu zangu ibada njema inaanzia nyumbani tukiendekeza vitendo hivi watoto wetu tunawafundisha nini? Waume zetu tunawapenda sana lakini ndoa ikiwa ndoano tusikubali kuvumilia matendo ya ukatili tuwashtaki waende wakajifunze” alisema Kusaduka.
Kwaupande wake Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Kata ya Uhuru, Haruna Ngereza aliwashauri watoto kuwa na nidhamu, kutojiingiza kwenye makundi mabaya na kushiriki matendo ya uhalifu kama wizi, ulevi na uvutaji bangi hali inayopelekea kupewa adhabu na kugeuza adhabu hizo kuwa ukatili wa kijinsia.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.