Na. Dennis Gondwe, MNADANI
Wazazi wa Kata ya Mnadani wametakiwa kuwa karibu na watoto wao ili kuwaepusha na kufanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia na kuwaathiri kisaikolojia.
Kauli hiyo ilitolewa na Diwani wa Viti maalum Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Fatuma Zollo alipokuwa akiongea na wakazi wa Kata ya Mnadani kuhusiana na madhara ya ukatili wa kijinsia katika jamii.
Zollo alisema kuwa wazazi wanawajibu mkubwa kuwakinga watoto dhidi ya ukatili wa kijinsia. “Sote tunatambua kuwa watoto wamekuwa wahanga wakubwa wa vitendo vya ukatili wa kijinsia. Njia pekee ya kuwasaidia watoto ni kuwa karibu yao na ili waweze kuwaeleza viashiria vya ukatili wa kijinsia wanavyokabiliana navyo mapema kabla hali haijawa mbaya. Ukatili wa kijinsia kwa watoto unawaathiri kimwili, kihisia na kisaikolojia. Baadhi ya watoto wamepoteza ndoto katika maisha yao kutokana na vitendo hivi” alisema Zollo.
Mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Kata ya Mnadani, Farida Mbarouk aliipongeza serikali kwa kutoa fedha nyingi za miradi ya maendeleo katika Kata ya Mnadani. “Serikali imefanya mambo makubwa sana kutujengea shule, vituo vya afya na mikopo ya asilimia 10 isiyo na riba inayotolewa na halmashauri ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM. Serikali imetujengea madarasa tisa na sasa shule mpya inajengwa. Utekelezaji huu utaongeza ufaulu kwa wanafunzi katika Kata ya Mnadani kwa sababu walimu wapo wa kutosha” alisema Mbarouk.
Alisema kuwa suala la ardhi lilikuwa changamoto kubwa. “Sasa ardhi inapimwa na watu wanamilikishwa viwanja. Suala la miundombinu ipo vizuri, barabara zinapitika muda wote. Maji yanapatikana kila siku” alisema Mbarouk.
Kwa upande wake mwananchi Aisha Juma alisema kuwa elimu ya ukatili wa kijinsia ni muhimu kwa jamii. Alisema kuwa Watoto wamekuwa wahanga wakubwa wa vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii na kushauri utoaji wa elimu dhidi ya ukatili iwe ajenda endelevu.
Madiwani 14 wa Viti maalum wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma wanafanya ziara katika kata 41 za jiji hilo kutoa elimu dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii na fursa za kiuchumi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.