Na. Dennis Gondwe, DODOMA
WAZAZI na wanafunzi wameshauriwa kujikita katika maombi ili Mungu aweze kufungua ufahamu utakaowawezesha wanafunzi kutumia maarifa waliyoyapata kipindi wakiwa shule katika kufaulu mitihani yao na kuwa raia wema.
Ushauri huo ulitolewa na Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Fungo alipokuwa akiongelea umuhimu wa maombi kwa wanafunzi wanaofanya mtihani wa taifa wa kidato cha Nne ofisini kwake.
Fungo alisema “maombi ni ile hali ya mtu kuzungumza na muumba wake. Watoto wetu waliopo shuleni wengi wanaimani na wanamuamini Mwenyezi Mungu, hivyo wanafahamu kuwa Mungu yupo. Mtu anapofanya maombi anaeleza mambo ambayo anahitaji ili Mungu amsaidie. Kipindi hiki cha mtihani wa taifa wa kidato cha Nne ni muhimu kwa wazazi kufanya maombi kwa ajili ya watoto wetu na watoto kwa sehemu yao wakamuomba Mungu awasaidie”.
Alisema kuwa vitabu vya dini vinaelezea wazi umuhimu wa kuitafuta elimu kwa nguvu na kuishika sana. “Mungu ndiye anatupa uzima, Mungu ndiye anatupa afya, Mungu ndiye anayetusaidia kwa kila jambo. Hivyo, ni muhimu kurudi kwa Mungu kumuomba ili awasaidie watoto wetu waweze kufanya vizuri katika mitihani yao. Wafanye vizuri kwa ajili ya faida yao na kwa ajili ya taifa lao. Sisi wazazi tunawategemea wao kuja kushika nafasi zetu ambao tayari tupo kazini. Tunawategemea kuja kushika nafasi za wafanyabiashara na nafasi mbalimbali kwa ajili ya ustawi wa familia zao na taifa lao” alisema Fungo.
Mkuu huyo wa Kitengo cha TEHAMA alisema kuwa kutokana na umuhimu huo, serikali inatoa fedha nyingi kugharamia elimu kwa lengo la kuwasaidia wananchi wake wapate elimu hiyo bila malipo ili kila mtoto apate fursa hiyo adhimu. Alisema kuwa wazazi wana wajibu wa kuunga mkono juhudi za serikali kuhakikisha watoto wanasoma na kufikia malengo yao na malengo ya taifa.
“Wanapoendelea na mitihani hii tunawatakia heri na mwenyezi Mungu awe pamoja nao awasaidie wakumbuke kila walichojifunza, Mungu awape hekima, ufahamu na maarifa waweze kufanya vema kwa faida ya taifa letu na faida ya familia zetu” alisema Fungo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.