Na. Dennis Gondwe, DODOMA
WAZAZI katika Wilaya ya Dodoma wametakiwa kuwajengea uwezo wanatoto wao ili waweze kujiamini na kujieleza ili waweze kutoa taarifa za vitendo vya ukatili wa kijinsia vinapojitoleza ili waweze kuwa salama.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri alipokuwa akifunga mashindano ya mdahalo kwa shule za sekondari zilizopo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma yaliyofanyika katika shule ya sekondari Dodoma.
Shekimweri alisema kuwa watoto wamekuwa wahanga wa vitendo vya ukatili wa kijinsia kutokana na kutokuwa na uwezo wa kujieleza. “Kama watoto wetu tukawafundisha na kuwajengea kujiamini na kujenga hoja ni ngumu mtu mwenye dhamira mbaya kufanya vitendo vya ukatili wa kijinsia” alisema Shekimweri.
Aliongeza kuwa tafiti zinaonesha kuwa miongoni mwa wanaosababisha ukatili wa kijinsia ni ndugu wa karibu wa familia. “Unakuta mjomba, baba mkubwa ndio wanaofanya ukatili kwa watoto. Hivyo, watoto wakiwa na kujiamini wataweza ‘kuraise voice’ kwamba vitendo hivyo havifai” alisema Shekimweri.
Kwa upande wake Mkuu wa Divisheni ya Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwalimu Upendo Rweyemamu alisema kuwa mashindano ya mdahalo kwa shule za
Halmashauri ya Jiji la Dodoma ngazi ya wilaya ni jambo jema. Aidha, aliagiza mashindano hayo yafanyike kwenye ngazi ya shule kati ya darasa na darasa ili kuwajengea wanafunzi uwezo wa kuzungumza na kuandika kwa lugha ya kiingereza.
Akiongelea umuhimu wa mdahalo katika taaluma, Rweyemamu alisema kuwa midahalo inamjengea mwanafunzi ujasiri wa kujielezea, kujenga hoja, inamuongezea misamiati ya lugha ya kiingereza, inamjengea ujasiri pia inaongeza ufaulu kwa wanafunzi.
“Tunaenda kuongeza ufaulu katika shule zetu sababu wanafunzi wanaenda kuwa vizuri kwenye lugha ya kiingereza, mwanafunzi anaweza akawa ameelewa swali lakini hana misamiati yakutosha ataishia kujua kichwani mwake lakini atashindwa kuweka kwenye maandishi kupitia midahalo mwanafunzi ataongeza misamiati na kumudu masomo yake pamoja na mitihani anayoulizwa kwa lugha ya kiingereza”, alisema Rweyemamu.
Mratibu wa mashindano ya mdahalo huo, Mwalimu Malick Masoud alisema kuwa mada zilizofanyiwa mdahalo huo zinalenga kupinga ukatili wa kijinsia. Alisema kuwa lengo ni kuona namna wanafunzi wanavyoshindwa kufikia malengo yao kutokana na ukatili wa kijinsia na namna ukatili huo unavyowaathiri.
“Watoto wanashindwa kufikia malengo yao kutokana na mambo ya ukatili wa kijinsia. Mashindano haya yana lengo mahususi la kuwasaidia wanafunzi kuchangamsha akili zao kwasababu wanakutana na wanafunzi kutoka shule mbalimbali na wenye uwezo tofauti, lakini pia yatasaidia kujenga uelewa wa masuala ya ukatili wa kijinsia na umuhimu wa utunzaji wa mazingira kutokana na mada walizozizungumzia katika mdahalo” alieleza Masoud.
Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Mnadani, Haruna Jumaa alishauri kwa wanafunzi wenzake kuchukua hatua wanapofanyiwa vitendo vya ukatili. Alisema kuwa ukatili hauwezi kuwa ukatili kama muathirika hataweza kutoa taarifa na hiyo hutokana na kutokujiamini. “Ukiona kitendo kinataka kutokea au kimekwisha kutokea toa taarifa kwa vyombo husika au hata kwa waliokuzidi umri ili waweze kupata namna ya kukusaidia” alisema Jumaa.
Mashindano hayo ya mdahalo yalianza tarehe 1 Oktoba, 2022 yakijumuisha shule 16 zilizopo ndani ya Jiji la Dodoma yalifikia ukomo jana na shule ya sekondari Miyuji kuibuka mshindi wa jumla.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.