WITO umetolewa kwa wazazi kuwapa nafasi Watoto washiriki kwenye michezo, kwa kuwa michezo ina faida kubwa kwenye makuzi na maendeleo yao kielimu.
Hayo yamesemwa na Afisa Elimu ya Sekondari wa Jiji la Dodoma, Mwalimu Upendo Rweyemamu katika siku ya mwisho ya mashindano ya UMISETA ngazi ya Wilaya yaliyofikia kilele chake katika uwanja wa Shule ya Sekondari Dodoma.
“Michezo na taaluma ni vitu viwili vinavyo enda pamoja unapo mruhusu mtoto kucheza anakuwa safi kiakili na kuchangamka kiasi kwamba anakuwa tayari kupokea ambacho anafundishwa na mwalimu wake, wazazi waacheni Watoto washiriki kwenye michezo”, alisema Rweyemamu.
Akifafanua zaidi Mwalimu Upendo Rweyemamu alisema mashindano hayo ya kutengeneza timu ya wilaya yameenda salama na tayari timu imekamilika ambapo mpaka kufikia tarehe 3 Juni wachezaji wa timu hiyo watatakiwa kuwasili kambini kwa ajili ya maandalizi kwa mashindano yajayo.
Mapema mgeni rasmi Mhe. Sospeter Mazengo ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya huduma za jamii, uchumi, elimu na afya wa Jiji la Dodoma ambaye alimwakilisha Mstahiki Meya aliwaeleza wanamichezo hao kuwa wale watakao chaguliwa kwenda mkoani kwa ajili ya kushindana na wilaya nyingine watambue wanajukumu la kuheshimisha Jiji kwa kufanya vizuri na kusisitiza kuwa wana nafasi ya kuyabadilisha maisha yao pia kwa kujituma, kuonesha vipaji na uwezo walionao.
Mazengo alisema kuwa michezo ni muhimu katika kulinda afya na ni njia ya kuingiza kipato ambapo ni vyema kufungua macho na kuweka nia katika kufikia malengo.
“Ukifanya tathimi timu ambazo zina shiriki ligi kuu idadi yake, wachezaji, waalimu na wadau mbalimbali wanao saidia timu kwa ujumla utabaini sekta ya michezo imeajiri watu wengi, hivyo kuna mlango, nawaambia ninyi ni vijana nafasi mnazo”, alisema Mazengo.
Kwa upande wake Mwalimu Shule ya Sekondari Viwandani Malick Masoud alisema kuwa watoto wana nidhamu ya kutosha na kata 41 zimeshiriki zikijumuisha shule 58 ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika mashindano ya UMISETA mwaka huu.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.