Na. Hellen M. Minja,
Habari – DODOMA RS
Kufuatia maelekezo aliyoyatoa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule juu ya wazazi kupeleka watoto shuleni pindi muhula mpya utakapoanza, leo Januari 15, 2025, Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma Bw. Kaspar K. Mmuya, amefanya ziara ya kikazi kutembelea shule ya msingi Kisasa kujionea utekelezaji wa maelekezo hayo.
Akiwa shuleni hapo, Katibu Tawala huyo alizungumza na walimu pamoja na wanafunzi juu ya umuhimu wa wazazi kuwaandikisha watoto wao mapema ili kutopunguza siku zao za masomo zilizopo kwenye kalenda ya mwaka.
“Elimu inatolewa kisayansi tukifahamu mwanafunzi katika mwaka mmoja anatakiwa kuhudhuria shuleni kwa idadi ya siku, na mtoto akihudhuria siku zote anaweza kupata kiwango kilichokadiriwa na walimu. Mzazi ukichelewa kumleta mtoto shule, jinsi unavyochelewa ndivyo idadi ya siku za mtoto kuhudhuria shuleni unavyozipunguza” Bw. Mmuya
Akitoa taarifa ya shule hiyo, Mwalimu Mkuu Bi. Jesca Mwarabu amesema shule yake ilianzishwa mwaka 2007, kwa sasa ina jumla ya wanafunzi 2,479 na walimu 57. Shule inatekeleza mtaala ulioandaliwa na Wizara ya Elimu na kwa miaka mitano mfululizo imekua na ufaulu mzuri kwa 90% na zaidi katika mitihani ya kumaliza elimu ya msingi huku uandikishaji wa darasa la awali na la kwanza 2025 ukivuka lengo kwa zaidi ya 100%.
Kwa upande mwingine, Kiongozi huyo amefanya ziara ya kukagua mradi wa ujenzi wa shule mpya ya msingi Sokoine (Mahungu) yenye mkondo mmoja, iliyopo katika Kata ya Nala Jijini Dodoma inayojengwa kwa fedha shilingi 321,800,000 kutoka programu ya BOOST kwa mwaka 2024/2025 ,na mradi upo kwenye hatua za umaliziaji.
Aidha, ziara hiyo ilitamatika kwa kutembelea Hospitali ya Wilaya ya Dodoma Mjini iliyojengwa katika Kata ya Nala ambapo mradi umetekelezwa kutokana na changamoto ya muda mrefu kwa wakazi wa Jiji la Dodoma kukosa Hospitali ya ngazi hiyo. Mradi umegharimu shilingi 1,500,000,000 fedha kutoka Serikali kuu na 480,000,000 kutoka Halmashauri ya Jiji na mpaka sasa mradi umekamilika kwa 98%
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.