WIZARA ya Afya kwa ushirikiano na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma imefanya uzinduzi wa kampeni ya chanjo dhidi ya ugonjwa wa Surua na Rubella inayotarajiwa kuanza kutolewa Februari 15 hadi 18, 2024 kwa watoto wenye umri kuanzia miezi 9 hadi miaka mitano(5).
Kampeni hiyo imezinduliwa rasmi kwenye ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa jengo la Mkapa Jijini Dodoma na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule.
Senyamule amewasisitiza wazazi wote wenye watoto wenye umri unaostahili kujitokeza kwa kwa wingi kuwapeleka watoto wao wapate chanjo hiyo.
“Tumekua tukipata chanjo hizi mara kwa mara kutokana na uhitaji ili kuepuka madhara yanayotokana na ugonjwa wa Surua. Nitoe Wito kwa wazazi wote wenye watoto wenye umri unaostahili kujitokeza kwa wingi wapate chanjo hiyo. Chanjo zimeandaliwa vizuri na kwa uhakika.
“Wakati wote Dodoma tumekua tukifanya vizuri kwenye chanjo hivyo hata wakati huu nitoe shime tufanye hivyo kwani Dodoma tumepewa heshima ya kufanya uzinduzi wa kampeni hii kitaifa siku ya Ijumaa. Tuwapeleke watoto kwenye vituo vya afya kwa tarehe zilizopangwa. Kwa pamoja tunaweza kutokomeza Surua na Rubella” Amesisitiza Senyamule.
Akitoa wasilisho la namna Mkoa uliyojipanga kufanikisha zoezi hili, Afisa chanjo Mkoa wa Dodoma Francis Bujiku, amesema;
“Tunatarajia kutoa chanjo hii kwa walengwa 426,964 na tayari dozi 469,660 zimeshasambazwa kwenye vituo vyote vya kutolea huduma hiyo ambavyo ni 543. Mradi huu imegharimu kiasi cha Shilingi 452,682,000.00 zilizotolewa na Shirika la GAVi chini ya Wizara ya Afya. Mpaka Sasa chanjo na vifaa vyote vimeshasambazwa”Bujiku.
Ugonjwa wa Surua na Rubella huambukizwa na virusi vinavyosambaa kwa njia ya hewa na dalili zake ni pamoja na homa, kikohozi, macho kuwa mekundu, vipele vidogo vidogo mwilini na n.k Magonjwa haya yanakingwa kwa chanjo tu. Chanjo hizi zinatarajiwa kutolewa kwenye vituo vya afya kwa huduma ya mkoba pamoja na klinik tembezi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.