WAZAZI wametakiwa kuzingatia unyonyeshaji bora na kuwapatia lishe bora watoto ili watoto wawe na afya bora na kuondokana na tatizo la udumavu wa akili na mwili.
Hayo aliyasema Muuguzi kutoka Zahanati ya Makole, Monica Isuja wakati wa Siku ya Afya na Lishe iliyofanyika katika Kata ya Mnadani, ambapo wazazi walipewa elimu ya unyonyeshaji bora na jinsi ya kuandaa lishe ya mtoto.
Alisema kuwa kuna wazazi ambao wanawapa watoto wao maziwa yenye maji ambayo sio mazuri katika makuzi ya mtoto lakini pia huwapatia vyakula vya aina moja visivyokuwa na lishe bora.
“Maziwa ya mwanzo baada ya mama kujifungua ni muhimu kwa mtoto kwasababu yana virutubisho vyote vyakutosha ambavyo humsaidia mtoto kukua vizuri na kumjengea Afya bora, lakini kuna vyakula ambayo ni maalum kwa watoto kuanzia umri wa miezi 6 hadi miaka mitano mfano wa vyakula hivyo, ni Mbogamboga, vyakula vya nafaka, matunda, nyama na vyakula jamii ya mikunde” alisema Isuji.
Aidha, Afisa Lishe Jiji la Dodoma, Neema Chaula alisema mjamzito anatakiwa kuzingatia siku 1000 za mwanzo kwasababu ndio kipindi ambacho mama anaweza kumtengeneza mtoto kiakili na kimwili.
“Mtoto akidumaa katika muda wa miaka miwili ni vigumu kumrekebisha na kuwa vyema tena. Hivyo, mama anatakiwa ahudhurie kliniki pindi anapojigundua kuwa mjamzito, kwasababu atapewa dawa maalum na elimu ya jinsi ya kutunza ujauzito mpaka kujifungua lakini pia kuzingatia ulaji ulio bora” alisema Neema.
Ikumbukwe kuwa kuna uhusiano mkubwa wa ukuaji wa watoto na lishe bora kwasababu mwili wa binadamu unajengwa ana vyakula vya aina tofautitofauti na virutubisho vya kutosha ili kuufanya mwili kuwa na nguvu na afya bora.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.