WAZAZI na walezi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma wametakiwa kuwa mstari wa mbele kuwatengenezea watoto wa kike mazingira rafiki wanapokuwa katika mzunguko wa siku za hedhi ili wasivuruge ratiba za masomo yao.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwalimu Upendo Rweyemamu alipokuwa akiongelea nafasi ya wazazi na walezi katika kumsaidia mtoto wa kike kuendelea na masomo anapokuwa katika mzunguko wa hedhi.
Mwalimu Rweyemamu amesema kuwa wazazi na walezi wanalo jukumu la msingi la kuwaelekeza Watoto wa kike kabla hawajaanza na wanapoanza mzunguko wa hedhi. “Wazazi, walezi na jamii kwa ujumla wanatakiwa kuwa mstari wa mbele kuwahamasisha watoto wa kike kutokupoteza vipindi vya shule wanapokuwa katika mzunguko wa hedhi. Lazima wawatengenezee mazingira sahihi Watoto wa kike kuelewa hali watakayokuwa nayo wakati wa hedhi” alisema Mwalimu Rweyemamu. Baadhi ya watoto wa kike wanapokuwa katika mzunguko wa hedhi hutumia siku nne hadi tano, hivyo kila mwezi mtoto wa kike anajikuta akipoteza wiki nzima ya kutohudhuria masomo, aliongeza. “Mzunguko huo unamfanya mtoto wa kike kupoteza siku nyingi za masomo. Wakati wenzake wanaendelea na masomo, wao wanakuwa wanakikosa masomo, na walimu hawawezi kurudi nyuma” aliongeza Mwl. Rweyemanu.
Aidha, aliwataka walimu katika Halmashauri ya Jiji kukumbuka kuwa Watoto wa kike wanapokuwa shuleni wanakuwa chini yao. “Walimu ndiyo wazazi kipindi watoto wa kike wanapokuwa shuleni. Hivyo, wanawajibu wa kuwaandalia sehemu maalum kwa ajili ya kujisitiri yenye usiri na usafi wa kutosha. Walimu wakiwatengenezea mazingira hayo, kutawawezesha watoto wa kike kuwa huru wakati wa masomo” aliongeza Mwalimu Rweyemamu.
Kwa upande wa watoto wa kike, aliwataka kufahamu kuwa mzunguko wa hedhi siyo ugonjwa, bali ni utaratibu ambao kila mwanamke lazima aupitie katika utimilifu wake. “Nichukue nafasi hii kuwashauri watoto wa kike wajitahidi wasibaki nyumbani, ili waweze kuhudhuria vipindi shuleni, ni kweli kuna maumivu wanayopitia kama kuumwa tumbo, kichwa na mgongo. Zipo njia za kawaida kupunguza maumivu hayo kama kunywa maji ya moto au kunywa maji mengi. Maumivu yanapozidi ni vizuri kufika katika vituo vya kutolea huduma za afya” alisisitiza Mwalimu Rweyemamu. Dhamira ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma ni kuona Watoto wote wa kike wakisaidiwa kipindi chote wanapokuwa katika mzunguko wa hedhi ili waweze kuhudhuria masomo yao katika juhudi za serikali kukuza na kuimarisha sekta ya elimu.
Ikumbukwe kuwa tarehe 28 Mei kila mwaka ni siku ya hedhi salama duniani ambapo jamii hujadili jinsi ya kutatua changamoto zinazowakabili wanawake na Watoto wa kike wanapokuwa katika mzunguko wa hedhi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.