Na. Theresia Nkwanga. DODOMA
AFISA Elimu Msingi Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Prisca Myalla amewataka wazazi kuwa karibu na walimu, kufatilia mienendo ya tabia za watoto wao ili kuwalinda dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Hayo ameyasema alipokutana na wazazi wa Kata ya K/Ndege katika shule ya msingi Mlimwa A iliyopo jijini Dodoma, kwaajili ya kuzungumza maswala mbalimbali ya malezi ya watoto, Lishe na namna ya kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia kwenye Kata ya K/Ndege.
Aidha, amewataka wazazi kufanya jukumu lao la malezi ya watoto nakuacha visingizo vyakushindwa kuwalea kwa sababu ya kutafuta fedha za kuendeshea Maisha.
‘’Tunapaswa kuwaelekeza hiki ni kizuri hiki ni kibaya, turudi kwenye misingi ya malezi ya watoto tufatilie mienendo ya watoto kupitia walimu wanaowafundisha hasa walimu wa darasa, fahamu marafiki zake ni kina nani, fahamu akiwa shuleni anatabia zipi na akiwa nyumbani anatabia gani na vilevile fahamu ratiba ya vipindi vya shule vinaisha saa ngapi. Niwasihi kina mama kuwaandaa watoto vile unavyotaka awe ni jukumu lako ukishirikiana na baba tuache visingizio vya kutafuta pesa huku tukiwaacha watoto wetu wanaangamia nakufanyiwa matendo maovu,” alisema Myalla
Akielezea namna ambavyo tunaweza wakinga watoto na vitendo vya ukatili Afisa Ustawi Wa Jamii Halmashauri, Recho Balisija alisema wazazi wanatakiwa kujenga tabia ya kukaa na kuzungumza na watoto wao,kushirikiana nao na kujenga urafiki na watoto ili wawe huru kuwataarifu pale wanapopitia changamoto yoyote na kuripoti wanapoona viashiria vya ukatili
‘’Turudi kwenye dini tuwalee watoto katika misingi ya dini, dini ni msaada mkubwa kwenye malezi ya watoto wetu, hakuna dini inayoruhusu ukatili tubebe watoto tuwapeleke kanisani tuwe na utaratibu wa kusali nao jioni, mtoto akilelewa katika imani atajifunza swala la ukatili ni dhambi Mungu hapendi’, aliongezea Basilija.
Naye, Afisa Maendeleo Dawati la Jinsia na Watoto Krista Kayombo, aliwaomba wazazi warudi kwenye mila na desturi zao za zamani wawarithishe watoto mila zilizo njema ili kukikomboa kizazi hiki cha sasa kinachoangamizwa na utandawazi.
‘’Wazazi wetu wazamani walikua na mila na desturi binti akivunja ungo anatakiwa kujistiri na haruhusiwi kuingia hovyo kwenye vyumba vya watoto wa kiume ila siku hizi watoto wakike wanavaa nguo zenye kuonesha maungo yao mbele za baba na kaka zao,” alisema Kayombo
Kwa upande wake James Magawa mzazi aliyehudhuria kikao hicho, aliwashauri wazazi kuwalea watoto katika misingi ya dini pia kuweka utaratibu wa kusali nao jioni ili kuwajenga watoto katika misingi ya kidini toka wakiwa wadogo alimalizia kwa kumshukuru Afisa elimu msingi kwa elimu aliyowapatia na kumuomba ikiwezekana hii elimu itolewe kuanzia ngazi ya shule.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.