Na. Dennis Gondwe, MAKUTOPORA
WAZAZI wametakiwa kuwa marafiki na watoto wao na kuwapa muda wakuwasikiliza ili waweze kufahamu changamoto wanazopitia kutokana na ukatili wa kijinsia.
Kauli hiyo ilitolewa na Diwani wa Viti maalum Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Asma Karim alipokuwa akiongea na wananchi wa Kata ya Makutopora jijini hapa kutoa elimu dhidi ya ukatili wa kijinsia.
Karim alisema “ndugu zangu wazazi mnatakiwa kuwa marafiki wa watoto wenu. Mpe mtoto dakika 10 kila siku kuzungumza nae tena ukimkazia macho usoni. Siyo wewe una ongea nae ukichati na simu, hapana. Simu ni nzuri lakini simu ukiitumia vibaya ni adui. Unamkuta mama na simu, simu na wewe hakuna kufanya kazi. Ndiyo maana watu wanakuwa hawashauriani nyumbani wala kufuatilia maendeleo ya watoto. Mazungumzo na mtoto yanasaidia kujua maendeleo ya mtoto wako kimasomo na kiafya”.
Alisema kuwa jukumu la kusomesha watoto ni wajibu. “Mtu yeyote asiyesomesha mtoto amemfanyia ukatili. Haki ya pili ni kumlinda asiathiriwe na masuala ya ukatili wakijinsia mpaka anafikisha umri wa kujenga mahusiano halali yanayokubalika. Mlinzi wa mtoto ni sisi wanajamii” alisema Karim.
Madiwani 14 wa Viti maalum wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma wanafanya ziara katika kata 41 za jiji hilo kutoa elimu dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii na fursa za kiuchumi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.