Na. Dennis Gondwe, DODOMA
WAZAZI na walezi wametakiwa kuwa karibu na watoto wao wanaofanya mtihani wa taifa wa kidato cha Nne mwaka 2022 wakiwasaidia na kuwatia moyo ili waweze kufanya vizuri katika mitihani yao inayoendelea nchi nzima.
Kauli hiyo ilitolewa na Afisa Elimu Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwalimu Upendo Rweyemamu alipokuwa akiongelea nafasi ya wazazi na walezi kwa watoto wanaofanya mtihani wa taifa wa kidato cha Nne mwaka 2022.
Mwalimu Rweyemamu alisema “nitoe rai kwa wazazi na walezi, hakuna kipindi kigumu kwa mwanafunzi kama kipindi hiki cha mtihani wa taifa, mtoto anaposikia mtihani anaogopa. Naomba wazazi na walezi kama kuna kitu mlikuwa hamkifanyi kwa watoto wenu kifanyeni sasa hasa wale watoto wanaotoka nyumbani. Mnaweza kuwaandalia chai na chakula jitahidi kuwa karibu na mtoto wako, mpe pole anapotoka kwenye mtihani, mfulie nguo zake ili mtoto ajisikie vizuri na hatimae kufanya vizuri katika mitihani yake”.
Halmashauri ya Jiji la Dodoma ina vituo 54 vitakavyofanya mtihani wa kidato cha Nne, ikiwa na jumla ya watahiniwa 6,647 ambao watafanya mtihani wa taifa wa kidato cha Nne, wavulana wakiwa 3,019 na wasichana 3,628.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.