WAZEE ni hazina kutokana na mchango wao katika kupigania uhuru na kutengeneza dira ya maendeleo kwa taifa.
Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi aliyekuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya wazee duniani ngazi ya Wilaya yaliyofanyika katika uwanja wa Nyerere square jijini Dodoma leo.
Katambi alisema “Umoja wa mataifa uliona umuhimu na mchango wa wazee duniani. Taifa lolote lililoendelea liliendelezwa na vijana wa wakati ule ambao ndiyo wazee wa sasa. Wazee ndiyo walipigana vita na kuleta uhuru. Wazee mnawajibu wa kushauri katika ngazi mbalimbali. Hata kwenye makanisa kuna wazee washauri. Ninyi ndio mnaotoa dira ya nchi hii”.
Serikali inatambua umuhimu wa wazee kama kundi muhimu katika jamii. Rais Dkt. Magufuli kwa kutambua umuhimu wa wazee alianzisha wizara inayogusa moja kwa moja masuala ya wazee ili kulinda stahili za wazee, alisema. “Serikali inaendelea kusisitiza na kutoa huduma bora kwa wazee. Katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, jumla ya vitambulisho 10,290 vimetolewa kwa wazee kwa ajili ya matibabu katika kata mbalimbali. Aidha, wazee 4,551 wamepatiwa misamaha ya tiba katika vituo vya afya” alisema Katambi.
Akiongelea hali ya tiba katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mkuu wa Wilaya alisema kuwa hali ya tiba ni nzuri. “Halmashauri imekuwa ikifanya vizuri katika kusimamia huduma za afya. Viongozi wote wakiongozwa na Mkurugenzi wa jiji wanafanya kazi kubwa kuhakikisha maslahi ya wazee yanalindwa” alisisitiza mkuu wa Wilaya.
Kwa upande wake, Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mhe. Emmanuel Chibago alisema “sehemu isiyokuwa na wazee hakuna hekima. Hekima ipo na wazee. Wazee ndiyo mnatakiwa kutulea sisi. Tunapoenda tofauti mtuite na kuturudisha kwenye mstari”. Aidha, aliwataka wazee hao kuwa na imani na serikali yao.
Katika risala ya wazee iliyosomwa na Katibu msaidizi wa baraza la wazee Wilaya ya Dodoma mjini, Veronica Mvutekule alisema kuwa wanaiomba serikali kuchukua hatua kali kwa familia zinazotelekeza wazee wao kwenye huduma za matunzo na makazi. “Tunaomba serikali ifikirie kuwapa wazee pensheni na mikopo isiyokuwa na riba. Tunaiomba serikali ituondolee kodi ya ardhi. Sheria ya wazee itungwe pamoja na kanuni zake” alisema Mvutekule.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.