WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Ummy Mwalimu ameliagiza Jiji la Dodoma kuunda chombo maalumu kwa ajili ya kusimamia uendeshaji wa miradi mikubwa ya kimkakati waliyonayo ikiwemo kituo kikuu cha mabasi yaendayo mikoani na nchi za nje cha Jijini Dodoma.
Pia ametaka mfumo wa utoaji huduma kituoni hapo uendelee kuwa rafiki kwa wateja, wajasiliamali, wafanyabiashara na wananchi wote kwa ujumla wanapopata huduma.
Waziri Ummy ametoa maagizo hayo Aprili 12, 2021 wakati alipofanya ziara katika kituo kikuu cha mabasi kilichopo eneo la Nanenane Kata ya Nzuguni Jijini hapa, ambapo alisema lazima kiundwe chombo kwa ajili ya kuendesha miradi hiyo ili iweze kuleta tija kwa nchi kama malengo yalivyokusudiwa.
“Kuna muongozo maalumu wa uendeshaji wa miradi hii, ili ilete tija, mimi nadhani kiundwe chombo maalumu cha kuendesha miradi hii ili tufikie lengo tulilokusudia, tunataka miradi hii izalishe mapato ili tukajenge shule, hospitali” alisema Waziri Ummy.
Alisema Serikali imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 24 katika mradi huo wa stendi hivyo mradi huo usimamiwe kikamilifu ili utoe huduma bora, huku akitaka mabasi yote yaanzie na kumalizia safari zake katika kituo hicho.
Waziri alisema Serikali ya awamu hii ikiongozwa na Rais wa sita wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan itaendelea kujali wafanyabiashara wadogo na kutaka wafanye biashara zao kwa amani na kwa kufuata sheria na taratibu wanazowekwa na mamlaka husika.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Joseph Mafuru alisema mpaka sasa mradi huo unasimamiwa na Jiji lakini wapo katika mchakato wa kuunda chombo kitakachosimamia na kuendesha miradi mikubwa ya kimkakati ya Jiji hilo ikiwemo kituo hicho, Soko Kuu la Job Ndugai na Hoteli ya kisasa yenye ghorofa 11 ya Dodoma City Hotel iliyopo katikati ya Jiji na wameshapeleka andiko ofisi ya Mkoa ili kubadilisha mfumo wa uendeshaji wa mradi huo na miradi mingine iliyopo katika jiji la Dodoma.
Naye meneja wa kituo hicho Abeid Msangi alisema kituo hicho kilianza kutoa huduma Juni 8, 2020 na kinauwezo wa kuhudumia mabasi mia moja (100) kwa wakati mmoja, na mpaka sasa tayari wameshakusanya shilingi milioni mia sita themanini (680,000,000) tangu kituo hicho kianze kufanya shughuli zake.
Ameongeza kuwa “kutokana na changamoto ya wafanyabiasha kutopanga maeneo yote ya biashara, tumeamua kushusha kodi ya pango kutoka shilingi elfu kumi na tano (15,000) ya awali kwa mita ya mraba hadi kufikia elfu kumi (10,000) ili tuwavutie wateja wengi zaidi kufanya biashara” alisema Msangi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.