WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Innocent Bashungwa ameziagiza halmashauri zote nchini kuhakikisha wanatekeleza mwongozo wa serikali wa kutotoza ushuru kwa wakulima wanaosafirisha mazao yao chini ya tani moja.
Bashungwa ameyasema hayo jana tarehe 8 Septemba 2022 jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa mwongozo wa kutotoza ushuru kwa wakulima wanaosafirisha mazao chini ya tani moja.
Amesema katika kuweka mazingira rafiki na wezeshi kwa wakulima, serikali ilitoa maelekezo ya kuhakikisha wakulima hawatozwi tozo wanaposafirisha mazao yao kutoka shambani kwenda kwenye magulio.
"Mpaka sasa bado maagizo ya Serikali ya kutotoza ushuru wakulima wanaposafirisha mazoa yao chini ya tani moja hayajabadilika. Bado maelekezo ya Serikali ni kuhakikisha wakulima wanapovuna na kupeleka mavuno ya mazao kwenye magulio na masoko kama ni chini ya tani moja wasitozwe ushuru wowote,"amesema.
Aidha, Bashungwa amemuagiza Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Profesa Riziki Shemdoe kuhakikisha mwongozo huo unazingatiwa na wakurugenzi wote nchini.
Bashungwa pia amewaelekeza Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kusimamia mwongozo huo katika maeneo yao.
"Nitumie nafasi hii kuwaelekeza wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya katika maeneo yao kusimamia jambo hili ili lisifanyike kiholela kwa maeneo mengine wanatoza na maeneo mengine hawatozwi, kwa hiyo kunakuwa na mkanganyiko upande wa wakulima lipi ni lipi,"amesema Bashungwa
Katika kutekeleza agizo hilo la Serikali, Ofisi ya Rais-TAMISEMI ilitoa mwongozo kwenye halmashauri zote namna ya kulitekeleza, hivyo niwakumbushe wakurugenzi kuendelea kuzingatia mwongozo huo na Wakuu wa Mikoa na Wilaya simamieni jambo hili lengo ni kumsaidia mkulima aweze kukua na kupambana na umasikini kupitia jasho lake la kilimo.
Aidha, Serikali iliona ni vyema kuhakikisha ushuru kwa mkulima wa mazao chini ya tani moja hautozwi na tunaendelea kuyasimamia kupitia wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kuhakikisha kwamba mwongozo huu unazingatiwa.
Chanzo: OR- Tamisemi
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.