WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jaffo amesema, Halmashauri ya Jiji la Dodoma ni ya mfano Nchini katika kuwatambua na kuwatengenezea vitambulisho maalum vya kuwatambulisha Wazee katika maeneo ya huduma mbalimbali ikwemo matibabu, akiwa ni utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Wazee ya mwaka 2003 inayolenga katika kuhakikisha kuwa, Wazee wa Tanzania wanatambuliwa na wanapewa fursa ya kushiriki katika mambo yanayohusu maisha ya kila siku na kupata huduma zote za msingi.
Waziri Jaffo ameyasema hayo mapema leo Mei 26, 2018, alipokuwa akizindua rasmi zoezi la utoaji wa vitambulisho vya Wazee kwenye hafla fupi iliyofanyika katika Kata ya Mkonze iliyopo umbali wa kilometa 4.7 kutoka katikati ya Jiji la Dodoma.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo ambayo pia ilihudhuriwa na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Deo Ndejembi na Mkurugenzi wa Jiji hilo Godwin Kunambi, Waziri huyo aliagiza Halmashauri za Mikoa yote 26 ya Tanzania Bara kuhakikisha zinawatambua Wazee katika maeneo yao na kuwasilisha taarifa kamili ya kila Mkoa kuhusu Wazee katika Ofisi yake ifikapo Juni 30, mwka huu.
Awali, akiwasilisha taarifa ya utekeleaji wa zoezi hilo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi, Mganga Mkuu wa Jiji hilo Hamadi Nyembea alisema Halmashauri ilianza zoezi hilo kwa kuwatambua Wazee katika Kata zote 41 za Jiji la Dodoma, na kwamba mpaka sasa jumla ya Wazee 15, 854 wameshatambuliwa kutoka katika Kata 33, sawa na asilimia 80.5.
Alisema, hatua iliyofuata ni kuwapiga picha Wazee waliotambuliwa na kuwatengenezea vitambulisho, zoezi lililoanza rasmi mwezi Februari Mwaka huu, ambapo jumla ya Wazee 1,118 wameshapigwa picha katika Kata za Mkonze, Mnadani, Uhuru, Madukani, Makole na Majengo na kwamba kazi hiyo inaendelea katika Kata zilizobaki.
“Jumla ya vitambulisho 564 vya Wazee vimeshakamilika na wahusika watakabidhiwa rasmi leo kwa ajili ya kuanza kuvitumia” alisema Mganga Mkuu huyo wakati akiwasilisha taarifa hiyo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.