Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo (Mb) ametangaza rasmi Uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika ngazi ya mtaa, kijiji na kitongoji unatarajiwa kufanyika Novemba, 24 mwaka huu.
Akitoa tangazo la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa mwaka 2019 katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa zilizoko katika Mji wa Serikali eneo Mtumba Jijini Dodoma Mhe. Jafo amewaagiza Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa kuhakikisha wanazingatia miongozo na kanuni za uchaguzi huo.
Mhe. Jafo amesema kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa za Mwaka 2019 ibara 4(1-3), Matangazo ya Serikali Na. 371, 372, 373 na 374) ya mwaka 2019, Waziri mwenye dhamana na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anautangazia umma wa Watanzania na Vyama vyote vya Siasa vyenye Usajili wa Kudumu kuwa tarehe 24 Novemba, 2019 itakuwa ni siku ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Tanzania Bara.
“Kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kifungu cha (1) Waziri mwenye thamana na Serikali za Mitaa anapaswa kutoa Tangazo la Uchaguzi kwa Umma si chini ya siku 90 kabla ya siku ya uchaguzi”. Amefafanua Mhe. Jafo
Mhe. Jafo ameeleza zaidi kuwa tarehe hiyo imepangwa baada ya kukamilika kwa kanuni ambazo zitatumika kuendesha uchaguzi huo ambapo wadau, vyama vya siasa na asasi za kiraia zilishirikishwa na kutoa maoni yao.
“Uchaguzi wa mwaka huu, utakuwa bora, kwa sababu umekuwa shirikishi wakati wa uandaaji kanuni na tumeandaa kanuni ambazo zinaondoa changamoto zilizokuwa zikijitokeza kwenye chaguzi zilizopita” Amesema Mhe. Jafo
Ameelezea kuhusu siku ya uchaguzi kuwa upigaji wa kura utaanza saa 2:00 asubuhi na kumalizika saa 10:00 jioni na watu watapiga kura kwa karatasi maalum ambazo zitatakiwa kutumbukizwa katika masanduku maalum ya kupigia kura
Ameendelea kufafanua kuwa kampeni za uchaguzi huo zimepangwa kufanyika kwa muda wa siku saba kabla ya uchaguzi, ambazo zitaanza Novemba 17 hadi 23 mwaka huu.
“Kampeni za Uchaguzi zitafanyika kwa muda wa siku saba kabla ya siku ya Uchaguzi. Ambapo kila Chama cha Siasa kinachoshiriki Uchaguzi kitawasilisha ratiba yake ya mikutano ya kampeni ya Uchaguzi kwa Msimamizi wa Uchaguzi si chini ya siku saba kabla ya kuanza kwa kampeni.” Amesema Waziri Jafo
Ameeleza kuwa nafasi zitakazogombewa ni Mwenyeviti wa Kitongoji katika Mamlaka za Miji Midogo, Mwenyekiti wa Mtaa na Wajumbe wa Kamati ya Mtaa (Kundi Mchanganyiko la Wanaume na Wanawake) na Wajumbe wa Kamati ya Mtaa (Kundi la Wanawake) katika Mamlaka za Miji.
Mhe. Jafo ameendelea kuzitaja nafasi nyingine kuwa ni nafasi za mwenyekiti wa Kijiji, Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji (Kundi Mchanganyiko la Wanaume na Wanawake), Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji (Kundi la Wanawake) na Wenyeviti wa Vitongoji katika Mamlaka za Wilaya.
Pia Mwenyekiti wa Kijiji, Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji (Kundi Mchanganyiko la Wanaume na Wanawake), Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji (Kundi la Wanawake) na Wenyeviti wa Vitongoji katika Mamlaka za Miji.
Kuhusu wagombea Mhe. Jafo amesema wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi watatakiwa kuwa wanachama na kudhamininiwa na Vyama vya Siasa vyenye Usajili wa Kudumu.
Waziri ameendelea kueleza kuwa ili kuwafahamisha wananchi majina ya maeneo na mipaka ambayo itahusika katika kujiandikisha na upigaji wa kura, msimamizi wa Uchaguzi atatangaza majina na mipaka ya Vitongoji vilivyoko katika eneo la Halmashauri husika siku 72 kabla ya siku ya uchaguzi kwa ajili ya Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kitongoji, Mwenyekiti wa Kijiji, Mwenyekiti wa Mtaa, Wajumbe wa Serikali ya Kijiji na Wajumbe wa Kamati ya Mtaa.
Amesema msimamizi wa uchaguzi atatoa maelekezo ya Uchaguzi siku sitini na mbili kabla ya siku ya uchaguzi na atafanya uteuzi wa watumishi wa umma watakaoandikisha na kuandaa Orodha ya Wapiga Kura siku 52 kabla ya siku ya Uchaguzi.
“Uandikishaji na uandaaji wa Orodha ya Wapiga Kura utaanza siku ya arobaini na saba (47) kabla ya siku ya uchaguzi na utafanyika kwa muda wa siku saba kwa kutumia fomu maalumu na utafanyika katika majengo ya umma na pale ambapo hakuna jengo la umma, uandikishaji utafanyika kwenye sehemu ambayo Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi atakuwa amekubaliana na Viongozi wa Vyama vya Siasa.
Waziri Selemani Jafo ameendelea kufafanua kuwa vituo vya kujiandikisha kupiga kura na kupigia kura, kwa maeneo yaliyo chini ya Halmashauri za Wilaya na Mamlaka za Miji Midogo vitakuwa katika ngazi ya Kitongoji na kwa upande wa Mamlaka za Miji (Miji, Manispaa na Majiji), vituo vya kujiandikisha kupiga kura na kupigia kura vitakuwa katika ngazi ya Mtaa
Amesema kuwa mtu anayekusudia kugombea nafasi za uongozi, atatakiwa kuchukua fomu ya uteuzi wa kugombea nafasi husika siku zisizopungua 26 kabla ya siku ya uchaguzi kwa kadri itakavyoelekezwa na Msimamizi wa Uchaguzi.
Hata hivyo, Kuhusu ukomo wa madaraka Mhe Jafo amesema kuwa viongozi wote walioko madarakani kwenye nafasi zote zitakazogombewa, uongozi wao utakoma siku 7 kabla ya siku ya kuchukua fomu za kugombea.
“Nafasi zote zinazogombewa zilikuwa na uongozi kwa kipindi cha miaka 5. Kwa mujibu wa Kanuni hizi, viongozi hao watakoma kushika nafasi za uongozi siku saba kabla ya siku ya kuchukua fomu za kugombea uongozi chini ya Kanuni hizi” Amesema Mhe. Jafo
Amesema mgombea amabye hataridhika na maamuzi ya msimamizi au msimamizi msaidizi wa uchaguzi kuhusu uteuzi atakata rufaa kwenye Kamati ya Rufaa inayopewa wajibu wa kusikiliza mapingamizi.
“Endapo wagombea hawataridhika na maamuzi ya Msimamizi au Msimamizi Msaidizi wa uchaguzi kuhusu uteuzi wa wagombea, kutakuwa na Kamati ya Rufaa katika kila Wilaya ambayo itasikiliza mapingamizi kuhusu uteuzi wa wagombea katika Wilaya husika” Amesisistiza Mhe. Jafo.
Wakati huohuo Mhe. Jafo amesema waangalizi wa ndani wa uchaguzi wanatakiwa kuomba kibali cha kufanya hivyo kwa katibu Mkuu Tamisemi kuanzia Agosti 26 hadi Septemba 16 mwaka huu ikiwa ni ndani ya siku 21 baada ya tangazo la uchaguzi kutolewa.
Aidha amewaomba wananchi wote kujitokeza kwa wingi kujiandikisha, kupiga kura, kugombea na kushiriki katika Uchaguzi huu ili kupata viongozi bora wa Serikali za Mitaa kwa maendeleo ya nchi yetu.
Halmashauri ya Jiji la Dodoma kama Mamlaka ya Serikali za Mitaa, tayari imeshaanza maandalizi ya kuhakikisha uchaguzi wa mwaka huu wa Serikali za Mitaa unafanyika kwa uwazi, utulivu mkubwa wa amani na kwa kufuata misingi ya demokrasia.
Chanzo: tovuti ya Wizara ya tamisemi.go.tz
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.