Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe Selemani Jafo amefurahishwa na hatua za awali za ujenzi wa Hospitali ya Uhuru inayojengwa katika eneo la Chamwino Mkoani Dodoma kwa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Magufuli.
Mhe. Jafo amesema amefanya ziara maalumu ya kukagua ujenzi wa Hospitali hii ya Uhuru tarehe 15 Julai 2019 baada ya kufika katika eneo hilo mnamo mwezi Juni na kutoridhishwa na hali aliyoikuta, ujenzi ulikuwa haujaanza na hata eneo lilikuwa halijasafishwa.
”Nilikuja hapa Juni 19 kukagua eneo hili sikuridhishwa baada ya kukuta ujenzi haujaanza, ndio maana nikatoa maelekezo kwamba ujenzi uanze mara moja kwa kutumia kikosi maalumu cha Jeshi ili kutimiza azma ya Mhe. Rais katika kutoa huduma bora za Afya karibu na wananchi, leo naona tayari wenzetu wa Suma JKT wameshaanza kazi hili limenifurahisha,” amesema Mhe Jafo.
Hivi ndio tunavyotakiwa tufanye kazi sio mnapewa maelekezo halafu mnaanza kujivuta vuta kufanya vikao visivyoisha hiyo haipendezi kwa sababu mnawacheleweshea wananchi huduma, aliongeza Jafo.
Nimefurahi zaidi kuona eneo lote la Ekari 40 limeshasafishwa ikiwemo kujenga uzio pamoja na ofisi za wafanyakazi wajenzi, pia vifaa vimeshaanza kufikishwa katika eneo hili la Hospitali na TBA wako wanaendelea na kazi yao ya usimamizi na ushauri hongereni kwa hilo alikazia Jafo.
”Kwa kweli leo nimeridhishwa na hatua ya awali ambayo tumefikia katika ujenzi wa Hospitali hii, na niwaombe wataalamu wangu kuacha kufanya kazi kwa mazoea na tunapotoa maagizo basi wayatekeleze kwa wakati, ni matarijio yetu hadi kufikia Januari, 2020 tutakua tumeshakamilisha ujenzi huu,” alisisitiza Mhe. Jafo.
Kwa upande wake Mhandisi kutoka Wakala wa Majengo Tanzania TBA, Mhandisi Daniel Mwakasungura amesema Hospitali hiyo ya Uhuru itakuwa ni ya gorofa moja na itatumia ramani ya Hospitali ya Tunduma iliyoboreshwa.
“Ramani iliyopendekezwa ambayo ni ya Hospitali ya Tunduma tunaendelea kuiboresha kulingana na mahitaji na viwango vya Hospitali ya Uhuru na sisi kama TBA tutasimamia suala la hili la ramani na kutoa ushauri wa mradi huu mpaka pale utakapokamilika” Alisema Mwakasungura.
Akizungumzia bajeti ya mradi mzima Mwakasungura amesema fedha iliyotengwa ambayo tumeingia mkataba na Suma JKT ni Shilingi Bilioni 3 ambazo zitajenga majengo yote yanayohitajika na tunatarajia mradi huu utakamilika baada ya miezi sita kama ambavyo tulievyoelekezwa,” amesema Mwakasungura.
Nae Mhandisi wa Suma JKT, Luteni Kanali Onesmo Njau amesema walikabidhiwa jukumu la ujenzi huo Juni 19 mwaka huu na tayari washatekeleza maelekezo kutoka kwa Mhe. Jafo ikiwemo kuandaa ofisi, sehemu za kuishi kwa watendaji na muda sio mrefu wataanza ujenzi ili kukamilisha mapema kama ilivyoelekezwa.
Hospitali hiyo inajengwa baada ya Rais Magufuli kuelekeza kufanya hivyo katika sherehe za Uhuru mwaka 2018 ambapo alifuta sherehe hizo na kupeleka Fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya sherehe hizo kujenga Hospitali ya Uhuru mkoani Dodoma.
Chanzo: tovuti ya OR-TAMISEMI (www.tamisemi.go.tz)
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.