Na. Dennis Gondwe na Sifa Stanley, DODOMA
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano na Mazingira, Selemani Jafo ameipongeza Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa juhudi zake za kuliweka jiji safi.
Pongezi hizo alizitoa mapema leo aliposhiriki zoezi la usafi pamoja na wananchi katika Soko la Bonanza Kata ya Chamwino Halmashauri ya Jiji la Dodoma
“Watu wa hapa mnafanya usafi kweli, sio kwa kuigiza. Nimetembea maeneo yote katika Samaki, Ndizi, Viazi pamoja na Matunda nimekuta mmefanya usafi. Ninyi ni watu wa kuigwa ndani ya Tanzania. Hii inadhihirisha kuwa maagizo ya Rais, Mama Samia na Dkt. Isdory Mpango akiwa yeye ni Makamu wa Rais na akisimamia upande wa Mazingira na Waziri Mkuu, wamekuwa wakitoa maelekezo kuhusu Mazingira na kufanya usafi, wanabonanza nimeshuhudia kwamba ni wasafi sana” alisema Waziri Jafo.
Pia Waziri Jafo alitoa wito kwa wananchi wa maeneo mengine kuzingatia maelekezo ya Serikali kuu ya kuacha biashara zao kwa muda mfupi na kufanya usafi siku ya Jumamosi. Sambamba na hilo alisisitiza watu wa maeneo mengine kuiga mfano wa Dodoma wa kuendeleza utamaduni wa usafi na kutunza Mazingira ili kuendelea kuiweka Nchi katika hali ya usafi.
“Niwaombe maeneo mengine waige mfano wa Dodoma, na Mkurugenzi wetu jambo hili liendelee katika masoko mbalimbali. Nafahamu wiki iliyopita tulikuwa na ajenda kama hii Soko la Majengo, leo hii tupo Soko la Bonanza inawezekana huenda Jumamosi ijayo tutakuwa Soko la Mavunde. Hili linawezekana tuwe tunabadilika, jiji letu tunafahamu ndio Makao Makuu ya nchi sura ya nchi yetu inapatikana Dodoma. Lazima tuhakikishe tunafanya usafi. Mimi kama Waziri wa Mazingira Tanzania hapa nimeridhika mnatunza Mazingira wanabonanza” alisema Jafo.
Nae Mkuu wa Idara ya Mazingira na udhibiti wa taka ngumu Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dickson Kimaro alisema kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma imekuwa na utaratibu wa kufanya usafi kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi na kuongeza kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma imetenga kiasi cha shilingi milioni 38 kwaajili ya kuboresha Soko la Bonanza.
“Katika Jiji la Dodoma tumekuwa tukifanya usafi kwa maelekezo ya mkuu wa mkoa kila Jumamosi tumekuwa tukifanya usafi isipokuwa Jumamosi ya pili ya mwezi huwa tunaiacha kwaajili ya maelekezo ya serikali kuu watu kufanya mazoezi. Soko la Bonanza ni moja kati ya masoko masafi kama alivyosema Afisa Mtendaji Kata ya Chamwino na Halmashauri ya Jiji la Dodoma imekuwa ikiendelea kuboresha mahali hapa na tumetenga shilingi milioni 38 kwa mwaka huu wa fedha wa serikali ili kuboresha soko hili” alieleza Kimaro.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.