WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo amesema Mradi wa Uimarishaji Mifumo ya Sekta ya Umma (Public Sector Systems Strengthening - PS3) umesaidia kudhibiti matumizi ya fedha na kuweka kumbukumbu sahihi za mapato katika vituo vya kutolea huduma.
Akizungumza na uongozi wa mradi huo, Jafo alisema umeimarisha mifumo ya TEHAMA ikiwemo iliyodhibiti matumizi ya fedha na kuweka taarifa sahihi za mapato katika vituo vya afya.
Ametoa mfano wa mfumo wa kielektoniki wa kuandaa mipango, bajeti na ripoti kwa Mamlaka ya Serikali za Mitaa (PlanRep), na kusema kuwepo kwa mfumo huo kumesaidia kuokoa Sh. bilioni nane zilizotumika kwa timu za bajeti za halmashauri wakati wa kukaa na kuandaa bajeti na kusafiri kwa ajili ya uwasilishaji rasimu za bajeti zao ngazi ya taifa.
"Kwa sasa hizo fedha zimeokolewa, kwani halmashauri zinatuma rasimu ya bajeti zikiwa katika maeneo ya kazi na kuifikia mikoani, hatimaye Tamisemi. Ikiwa kuna maboresho yanafanywa kupitia teknolojia," alieleza.
Kuhusu Mfumo wa Uhasibu wa Utoaji wa Taarifa za Fedha kwenye vituo vya kutolea huduma, Jafo alisema kwa sasa fedha zinazowasilishwa katika vituo vya afya na shule zimekuwa na uwazi, kwani pindi wanapozipokea hufanya matumizi kwa kuzingatia taratibu za fedha kupitia mfumo huo.
Kutokana na mafaniko hayo, alipongeza mradi huo. Aidha, alieleza kuwa pongezi hizo hawezi kuzitoa mikono mitupu hivyo kuwakabidhi vyeti vya kuthamini mchango uliotolewa katika ofisi ya TAMISEMI.
“Cheti kimoja ni kwa ajili ya Shirika la Misaada ya Maendeleo ya Kimataifa (USAID) ambao ndio wamekuwa wakitoa fedha na cheti kingine ni kwa ajili yenu PS3 ambao mmekuwa watekelezaji wa kazi za mradi huo,” alieleza.
Alisema ofisi yake inajivunia kushikirikiana na PS3 katika kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi kwa sababu kazi inayofanywa na mradi huo imewezesha kuwa na serikali yenye uwazi, maendeleo endelevu na ustawi wa pamoja.
Mkurugenzi wa mradi wa PS3, Dk Emmanuel Malangalila aliishukuru serikali kwa ushirikiano inaowapa wakati wote wa utekelezaji wa kazi za mradi huo.
Dk Malangalila aliongeza kuwa mradi huo unatekelezwa katika mikoa 13 Tanzania Bara lakini kazi zilizofanywa zimegusa mikoa yote 26 kutokana na uhitaji na umuhimu wa kazi za mradi katika kila mkoa.
PS3 inayofadhiliwa na USAID inafanya kazi katika mikoa 13 na halmashauri 93 Tanzania Bara ikiwa na lengo la kuimarisha huduma za umma kwa njia ya utawala bora, mifumo ya mawasiliano, fedha, rasilimali watu, pamoja na tafiti tendaji.
Chanzo: www.habarileo.co.tz
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.