HALMASHAURI ya jiji la Dodoma imetakiwa kujenga shule ya msingi ya mfano kwa kuzingatia viwango na ubora ili iwe alama kwa Taifa na kukidhi dhana ya kuiita shule ya mfano.
“Ujue mpaka shule inapewa hadhi ya kuwa ya mfano inatakiwa iwe ya utofauti mkubwa sana na shule za kawaida kuanzia kwenye ramani ya majengo, ukubwa wa eneo, muonekano wa majengo yanayojengwa, mandhari, viwanja vya michezo na kila kitu kitakachowekwa katika shule hiyo” Alisema Jafo
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Selemani Jafo (Mb) alipofanya ziara ya kazi kutembelea ujenzi wa shule ya msingi ya mfano inayojengwa katika Kata ya Ipagala jijini hapa jana.
Jafo alisema kuwa shule ya msingi ya mfano inatakiwa kuwa katika viwango na ubora wa juu ili kuwa ‘icon’ ya taifa katika ujenzi wake. “Shule ya mfano, nataka vitu vyote viweze kuwepo. Shule hii siyo ya Prof. Mwamfupe (Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma) amekaa na Baraza lake la Madiwani wameamua kuja kujenga shule. Hii ni shule ambayo ni ‘icon’ kwa Taifa letu, tuweze kuiona” alisema Jafo.
Aidha, aliipongeza Halmashauri ya Jiji kwa kukidhi vigezo vya ukubwa wa eneo kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo. “Hapa mmefaulu kwa vigezo vya ukubwa wa eneo, nataka mtu akija aone kweli hii ni shule ya msingi ya mfano” alisisitiza Jafo.
Awali Afisa Elimu ya Msingi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mabeyo akitoa taarifa ya ujenzi huo alisema kuwa, Halmashauri ilipokea fedha kiasi cha shilingi 706,400,000 kutoka serikali kuu kwa ajili ya ujenzi wa shule ya msingi ya mfano. Mabeyo alieleza mchanganuo wa matumizi ya fedha hizo kuwa ni kujenga vyumba vya madarasa 17 (Tshs 340,000,000), kujenga maktaba moja (Tshs 50,000,000), kujenga bwalo la chakula (Tshs 100,000,000), kujenga nyumba mbili za familia mbili mbili (100,000,000), kujenga matundu 34 ya vyoo (Tshs 37,400,000) na kujenga jengo la utawala (Tshs 50,000,000).
Akiongelea hatua ya utekelezaji, Afisa Elimu huyo alisema kuwa madarasa tisa yameanza kujengwa kuta zake baada ya hatua ya jamvi kukamilika, madarasa matano yamemwagwa jamvi na madarasa mawili yamejengwa msingi. Jengo la Bwalo la chakula limejengwa msingi na kazi inaendelea, pia nyumba mbili za walimu. Kuhusu ujenzi wa maktaba na jengo la utawala, Mabeyo alisema nondo na mawe kwa ajili ya jamvi vimeshaandaliwa.
Aidha, Mabeyo aliitajaa changamoto ya upatikanaji wa kokoto kwa ajili ya ujenzi. Alisema hali hii imesababishwa na kasi kubwa ya ujenzi katika jiji la Dodoma kwa kuwa taasisi nyingi za serikali, taasisi za binafsi, mashirika na watu binafsi wengi wamekuwa wakiendesha shughuli za ujenzi katika jiji la Dodoma kutekeleza adhma ya Serikali kuhamia Mji Mkuu Dodoma. Hata hivyo alisema bado kazi ya ujenzi wa shule ya mfano imekuwa ikiendelea vizuri.
Waziri Sulemani Jafo mwenye chepe, Mkuu wa Mkoa Dkt. Binilith Mahenge (aliyevaa track suit) na Mkuu wa Wilaya Protas Katambi wakishiriki kazi za ujenzi wa shule ya mfano walipotembelea kuona maendeleo ya kazi ya ujenzi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.