WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Seleman Jafo ameiagiza Halmashauri ya Jiji la Dodoma kujenga uzio wa ukuta kuzunguka moja ya bwawa la maji machafu lililopo katika dampo la kisasa la Chidaya jijini hapa ili kuepusha uwezekano wa watu kutoka nje ya eneo la bwawa hilo kuingia au uchafu kutoka nje na kuleta madhara kwa Wananchi wanaozunguka eneo hilo.
Waziri Jafo ameyasema hayo leo alipotembelea dampo hilo na kujionea kazi za udhibiti wa taka zinazozalishwa Jijini hapa ambazo zinafanyika katika eneo hilo.
Waziri huyo ameongeza kuwa dampo hilo linatakiwa kuwa msaada kwa wakazi wa Dodoma na sio kero, hivyo mamlaka husika zinatakiwa kuwa macho usiku na mchana kuhakikisha hakuna madhara yeyote yanayowapata wananchi pembezoni mwa dampo hilo.
"Mwananchi yeyote akidhurika sisi wote hapa tutaulizwa kuwa nyinyi kama viongozi mlipewa dhamana ya kuwalinda wanachi lakini kinyume chake mmeacha wanateseka, kwa hiyo nawaomba muwajibike na ninatoa mwezi mmoja na nusu ukuta huo ukamilike" alisema Waziri Jafo.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Mazingira na udhibiti wa taka ngumu wa Jiji la Dodoma, Dickson Kimaro alisema kuwa ameyapokea maelekezo hayo na ameahidi kuyafanyia kazi.
Aidha, Kimaro amemhakikishia Waziri wa Mazingira kuwa hakuna mwananchi yeyote atakaedhurika au kukumbwa na madhara katika eneo hilo kwani wamejipanga kutunza mazingira na watu wanaozunguka dampo hilo kwa ujumla.
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Seleman Jafo (wa kwanza kushoto) akisikiliza maelezo kuhusu Dampo la Kisasa la Chidaya kutoka kwa Mkuu wa Idara ya Mazingira na Udhibiti wa Taka ngumu wa Jiji la Dodoma, Dickson Kimaro leo 23 Aprili, 2021 wakati Waziri alipofanya ziara kutembelea dampo hilo.
Waziri Seleman Jafo (mwenye suti) akiongozwa na Mkuu wa Idara ya Mazingira wa Jiji la Dodoma, Dickson Kimaro (kulia) na Meneja wa Dampo la Chidaya, John Kiwanga (kushoto) wakati Waziri alipofanya ziara kutembelea dampo hilo la Jiji la Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.