Waziri wa TAMISEMI Mhe. Sulemani Jafo mnamo March 14, 2019 katika ukumbi wa NSSF uliopo Manispaa ya Kigoma/Ujiji amezindua Mfumo wa Taarifa za Kijiografia (GIS) uliofadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia Mradi wa Kimkakati wa Ukuzaji wa Miji na Majiji Tanzania (TSCP).
Akihutubia katika ukumbi huo alisema mfumo huo utasaidia katika ukuzaji wa mapato kwa halmashauri na namna ya kuwahudumia wananchi waliopo katika Manispaa hiyo kutokana na mfumo huo kuwa na taarifa mbalimbali zitakazoanza kukusanywa kutoka kwa makazi yote, biashara na huduma za jamii zilizopo katika eneo husika.
Alisema Manispaa ya Kigoma/Ujiji ndio imekuwa sehemu ya kuandalia mfumo huo ikiwa imepangwa kutumika katika halmashauri nane zinazopitiwa na mradi wa TSCP na kufadhiliwa na Benki ya Dunia huku akiwataka watendaji kujifunza Mfumo huo na kuhakikisha wataalamu wa Tehama waliopo katika halmashauri zote nane wanatoa ushirikiano katika mfumo huo.
Halmashauri nane zinazopitiwa na Mradi wa Kimkakati wa Ukuzaji wa Miji na Majiji Tanzania (TSCP) ni Halmashauri za Majiji ya Dodoma, Mwanza, Mbeya, Arusha na Tanga, zingine ni Halmashauri za manispaa ambazo ni Ilemela, Kigoma-Ujiji na Mtwara-Mikindani.
Akiendelea kuhutubia aligusia suala la upotevu wa mapato kutokana na upotevu wa mashine za kukusanyia mapato (POS) huku akiasa halmashauri kuchukua hatua za kimaadili katika upotevu huo na kuonya halmashauri katika utumiaji wa fedha mbichi ambazo zinakuwa hazijafuata taratibu katika kufikia matumizi.
Naye Mhandisi Mussa Nati ambaye ni mhandisi na mtaalamu wa mfumo wa GIS kutoka Benki ya Dunia alisema mfumo huo tayari umeshaanza kutumika katika wilaya ya Kinondoni na umeleta tija katika ujenzi wa barabara na jinsi ambavyo hakukuwa na tatizo la migogoro ya fidia kwa wakazi. Aidha, alieleza kuwa umeweza kukuza mapato katika wilaya hiyo na ametoa rai mfumo huo utumike vizuri na kuulinda kupitia wataalamu waliopo.
Naye meya wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji Mhe. Hussein Ruhava alishukuru kwa uzinduzi huo kufanyika katika manispaa hiyo huku akisema ni heshima kubwa ambayo serikali imeitoa na ameahidi kutoa ushirikiano na madiwani wote katika ukusanyaji wa mapato kutokana na mfumo huo na kuitaka serikali kuitazama zaidi manispaa hiyo kutokana na uwepo wa huduma duni zilizopo.
Naye mkuu wa wilaya ya Kigoma kwa niaba ya Mkuu wa mkoa ametoa salamu na kusema ofisi ya Mkuu wa mkoa itatoa ushirikiano kwa kusimamia na kuhimiza halmashuri kutumia mfumo huo kwa usahihi.
Waziri Jafo baada ya kumaliza mkutano huo katika ukumbi wa NSSF ambapo viongozi mbalimbali walihudhulia kutoka ofsi ya Mkuu wa mkoa, Wakuu wa wilaya zote za mkoani Kigoma, wakurugenzi wa Halmashauri, Meya wa manispaa ya Kigoma/Ujiji, Mkurugenzi wa Kigoma/Ujiji, Madiwani, wataalamu, wenyeviti wa mtaa pamoja na waandishi wa habari alifanya ziara katika eneo la Msimba lilipo dampo la taka la manispaa ambapo alitoa tamko kuanza kutumika kuanzia sasa.
Chanzo cha habari: Mhandisi Emmanuel Manyanga
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.