WAZIRI wa Nchi OWM - Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenister Mhagama ameitaka jamii kuacha kuwatumia watu wenye ulemavu kama chanzo cha mapato na badala yake jamii iwasaidie ili nao waweze kufikia malengo yao kimaisha.
Waziri Mhagama ameyasema hayo jana wakati wa zoezi la kugawa miguu bandia kwa wananchi 50 wa Jijini Dodoma katika hafla fupi iliyofanyika katika Hotel ya Dodoma kufuatia ufadhili wa Taasisi ya Kamal Group.
Akizungumza katika Hafla hiyo, Waziri Mhagama ameipongeza Taasisi ya Kamal Group kwa kufadhili miguu hiyo na kuwaomba kuwafikia watu wengi zaidi wenye uhitaji katika maeneo mengi ya Tanzania kama walivyofanya Dodoma Mjini na ametumia fursa hiyo pia kumpongeza Mbunge Mhe. Anthony Mavunde kwa kuwa bega kwa bega na watu wenye ulemavu katika kuwasaidia kutatua changamoto zao.
“Serikali itahakikisha inachukua hatua kali kwa wale wote ambao watawatumia watu wenye ulemavu kama chanzo cha mapato, tutaendelea na msako ili kuwabaini wahusika na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria”. Alisema Waziri Mhagama
Akitoa salamu zake, Naibu Waziri anayeshughulikia watu wenye ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga ametoa rai kwa Taasisi na watu binafsi kuiga mfano wa Kamal Group kwa kusaidia kutatua changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu.
Naye Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mhe. Anthony Mavunde ameishukuru Taasisi ya Kamal Group kwa ufadhili huo wa miguu na kuwataka wanufaika wote watumie viungo hivyo kama kichocheo cha kujiletea maendeleo yao na kuahidi kuwasimamia katika kupata mikopo itolewayo na Halmashauri ya Jiji la Dodoma kutoka kwenye mapato ya asilimia 2 vya mapato yake ya ndani.
Akitoa salamu kwa niaba ya Kamal Group, Bi. Hedwick Peter ameihakikishia serikali juu ya dhamira ya taasisi hiyo kuendelea kuigusa jamii yenye mahitaji kwa kutoa miguu na vifaa saidizi ikiwa ni sehemu ya utaratibu ambao taasisi hiyo imejiwekea kutekeleza sera ya kurudisha kwa Jamii (CSR) ambapo mpaka hivi sasa zaidi ya miguu 350 imetolewa kwa wahitaji mbalimbali.
Tazama picha mbalimbali wakati wa tukio hilo:
Chanzo: @anthonymavunde (instagram)
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.